Polisi wawasaka washukiwa baada ya 2 kuuawa, 28 kujeruhiwa katika shambulizi la bunduki mjini Baltimore, Maryland

Afisa wa Polisi asimama katika eneo palipotokea shambulizi la Bunduki mjini Baltimore, Maryland.

Maafisa wa Baltimore, jimbo la Maryland, Marekani, wanaendelea kuwatafuta washukiwa wa shambulizi lililotokea mapema Jumapili, wakati wa sherehe zilizofanyika katika mtaa mmoja mjini humo.

Polisi walisema kwamba takriban watu wawili waliuawa na wengine 28 kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi wakati wa sherehe kwenye mtaa wa kusini mwa mji huo, wa Brooklyn Homes.

Ripoti za polisi zimesema kwamba watatu miongoni mwa waliojeruhiwa wapo katika hali mahututi.

Meya wa Baltimore Brandon Scott ameambia vyombo vya habari kwamba tukio hilo linaangazia umuhimu wa kushughulikia tatizo la umiliki wa bunduki, na siyo mjini humo pekee mbali kote nchini. K

aimu mkuu wa polisi wa Baltimore Richard Worley, amesema kuwa watu 20 miongoni mwa waliojeruhiwa waliweza kutembea wenyewe hadi hospitalini.

Katika hotuba yake, Meya Scott alisema hawatapumzika hadi wapate waliofanya ukatili huo.

Ameongeza kwamba anatumai waliohusika wanafikiria kuhusu kila mtu ambaye maisha yake wameyakatiza. Mamlaka zilizema angalau watu wawili walifyatua risasi kwenye shambulizi hilo, lakini huenda idadi ya waliohusika ikawa kubwa Zaidi.