Watu 19 wameuawa katika shambulizi la Israel lililolenga msikiti - Maafisa wa Palestina

  • VOA News

Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa Israel Ben-Gvir

Maafisa wa Palestina wanasema shambulizi la Israel dhidi ya msikiti katika Ukanda wa Gaza limesababisha vifo vya takriban watu 19.

Israel wakati huo huo ilizidisha mashambulizi yake ya mabomu kaskazini mwa Gaza na kusini mwa Beirut siku ya Jumapili katika hatua ya kuzidisha vita dhidi ya makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran katika eneo zima.

Watu waliokimbia makazi yao walikuwa wanapata hifadhi katika msikiti huo uliopigwa karibu na hospitali kuu katikati mwa mji wa Deir al-Balah. Watu wengine wanne waliuawa katika shambulizi dhidi ya shule inayohifadhi watu waliokimbia makazi karibu na mji huo.

Jeshi la Israel limesema mashambulizi yote mawili yalilenga wanamgambo, bila kutoa ushahidi.

Israel inaendelea kupambana na Hamas huko Gaza mwaka mmoja baada ya shambulio la kundi hilo dhidi ya Israel lililotokea tarehe saba mwezi Oktoba mwaka jana, na imeanzisha awamu mpya ya mashambulizi nchini Lebanon dhidi ya Hezbollah, ambayo imekuwa ikikabiliana na Israel katika maeneo ya mpakani tangu vita vya Gaza kuanza. Israel pia imeapa kuishambulia Iran yenyewe baada ya Tehran kufanya shambulio la kombora la balestiki katika nchi hiyo wiki iliyopita.