Watu 18 wafariki katika ajali ya mlipuko wa kiwanda fataki Thailand

Eneo la kiwanda ambapo ilitokea ajali ya mlipuko wa fataki karibu na mji wa Sala Khao, mkoa wa Suphan Buri , nchini Thailand, Jan. 17, 2024. (Photo by handout/Thailand Novice Kaew Suphanburi Highway Rescue Association/AFP)

Watu wasiopungua 18 wamefariki baada ya mlipuko kutokea katika kiwanda cha fataki katikati mwa mji wa Thailand Jumatano, mfanyakazi wa uokoaji alisema.

“Watu 18 waliokutwa wamefariki, walithibitishwa,” mfanyakazi huyo alisema.

Mlipuko huo ulitokea kiasi cha saa tisa mchana (0800GMT) karibu na kitongoji cha Sala Khao, katika jimbo la kati la Suphan Buri.

Polisi wameliambia shirika la habari la AFP mamlaka ilikuwa inaendelea kupata idadi rasmi ya vifo hivyo.

“Kulikuwa na vifo, tunaangalia watu wangapi wamefariki,” kanali wa polisi Theerapoj Rawangban aliiambia AFP.

“Hatuoni uharibifu zaidi katika majumba mengine au watu wanaoishi (karibu) na jamii hiyo,” alisema.

Hakuna ishara yoyote ya kile ambacho huenda kimesababisha mlipuko huo.

Picha zilizosambazwa na huduma ya uokozi wa eneo hilo zilionyesha kifusi cha chuma kikiwaka moto ardhini, na moshi mweusi umetanda.

Milipuko katika karakana za kutengeneza fataki na aina kama hizo siyo vitu vigeni nchini Thailand.

Watu kumi walifariki, na zaidi ya 100 kujeruhiwa, baada ya mlipuko kutokea katika ghala la fataki huko mjini Sungai Kolok katika jimbo la kusini la Narathiwat mwaka 2023.

Ufalme wa Asia Kusini Mashariki pia ina rekodi mbaya ya usalama katika sekta ya ujenzi na ajali mbaya ni kitu cha kawaida kutokea.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.