Mashabiki walipiga makofi, walishangilia na kuimba pamoja na wanamuziki zaidi ya 20 akiwemo muimbaji nyota wa Senegal Didier Awadi ambaye aliuambia umati wa watu waliojaa furaha uliohudhuria hafla hiyo katika jiji la Bukavu kuwa "Dhamira yetu ni kuwa pamoja nanyi.”
“Tuna jukumu la kuonyesha mshikamano, kuwa upande wa watu wanaoshambuliwa” Awadi aliliambia shirika la habari la Reuters baada ya onyesho.
Tamasha la Amani, kwa kawaida hufanyika Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Lakini tamasha hilo lilihamishiwa sehemu nyingine kwa mara ya kwanza tangu lizinduliwe mwaka 2014, kutokana na mashambulizi ya kundi la waasi wa M23, ambao wamelikaribia jiji hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Bukavu ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, unaoonekana kuwa salama zaidi, licha ya kuwepo kwa makundi kadhaa yenye silaha. Zaidi ya watu 30,000 walihudhuria tamasha hilo, ambalo lilifanyika kuanzia Ijumaa hadi Jumapili.
-Chanzo cha habari hii inatoka shirika la habari la Reuters