Warepublikan kukutana faragha kupiga kura kufikia makubaliano nani awe mgombea wa nafasi ya uspika

Jim Jordan (kushoto) na Steve Scalise

Warepublikans katika Baraza la Wawakilishi la Marekani wanatarajiwa kukutana Jumatano katika kikao cha faragha, kupiga kura kati yao ili kujaribu kukubaliana juu ya mgombea ambaye atakuwa spika ajaye wa Bunge

.Wagombea wawili wa juu, Wawakilishi Jim Jordan na Steve Scalise, walihutubia wanachama wa chama chao katika mkutano uliofanyika Jumanne jioni wakiwasilisha hoja yao ya kuchukua nafasi hiyo ya uongozi baada ya aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy kuondolewa madarakani wiki iliyopita.

McCarthy aliwaambia wenzake wasimpendekeze katika kinyang’anyiro hicho kurudi kugombea tena.

Warepublikan wana wingi mdogo wa 221-212 katika Baraza hilo ikimaanisha kuwa itawabidi wote wakubaliane kumuunga mkono mgombea mmoja ili waweze kufikia idadi ya ushindi wa wingi mdogo kumchagua spika.

McCarthy alihitaji duru 15 za upigaji kura kushinda mwezi Januari wakati Wademokrat walipokuwa wakimuunga mkono mgombea wao, kiongozi wa Wademokratik katika Baraza Hakeem Jeffries, huku baadhi ya Warepublikan wakizuia kura yao mpaka pale McCarthy alipokubali kutekeleza baadhi ya matakwa yao.

Moja kati ya makubaliano hayo ni kumruhusu mwakilishi yeyote kuwasilisha hoja ya kumuondoa na kulazimisha kuwepo kura kama spika aondolewe. Mwakilishi wa Republikan Matt Gaetz aliwasilisha hoja baada ya McCarthy kutegemea kura za Wademokrat kuzuia serikali kufungwa.

Nafasi ya spika kuwa wazi kumefanya shughuli katika Bunge kusimama, huku tarehe ya mwisho ya katikati ya Novemba ikitegemea kumalizika kwa miswaada kadhaa ya kufadhili serikali ili kukamilika au mara nyingine tena kuwepo uwezekano wa serikali kufungwa. Msaada kwa Ukraine pia unasubiri kuidhinishwa.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.