Kesi hizo zinapinga kanuni mbalimbali zinazo simamia uchaguzi, nyingi kati ya hizo zikijikita katika kupiga na kuhesabu kura zinazotumwa kwa njia ya posta ambazo zimekuwa na mvuto zaidi katika miaka ya karibuni.
Hadi kufikia Jumatatu, jumla ya kesi 128 zinazohusiana na uchaguzi na upigaji kura zimefunguliwa mpaka sasa mwaka 2022, kulingana na mtandao wa Democracy Docket, taasisi ya mrengo wa kushoto inayofuatilia haki za kupiga kura ambayo hufuatilia mashtaka ya uchaguzi. Kati ya jumla hiyo, kesi 71 zinahusu kuzuia watu kupiga kura, nyinginezo zinalenga kupanua au kulinda haki ya kupiga kura, Democracy Docket imesema.
Uchambuzi wa mwezi Septemba wa Democracy Docket unaonyesha kuwa Warepublikan walikuwa na zaidi kidogo ya nusu ya hizo kesi zilizofunguliwa mwaka huu.
Sylvia Albert, Mkurugenzi wa Upigaji Kura na Uchaguzi katika taasisi ya Common Cause, taasisi ya uangalizi isiyofungamana na siasa na ya utetezi, ilisema kiwango kisicho cha kawaida cha kesi kitaweza kuufanya uchaguzi wa katikati ya muhula kuwa wenye mengi zaidi katika kumbukumbu ya hivi karibuni, baada ya uchaguzi pekee wa urais wa 2020.
“Ni kawaida kuwepo kwa kiwango kidogo cha kesi kadhaa kwa pande zote ili kupata ushindi,” Albert alisema. “Kile ambacho ni tofauti wakati huu wa uchaguzi ni kuwepo tu kesi kadhaa na jaribio la wazi la kuwanyang’anya haki wapiga kura na kukandamiza imani ya watu kuhusu uchaguzi.”
Katika uchaguzi wa 2020, Democracy Docket ilifuatilia kesi 68 zilizokuwa zimefunguliwa kabla ya Siku ya Uchaguzi.
Hans von Spakovsky, meneja wa juhudi za mageuzi ya sheria ya uchaguzi katika Taasisi ya Heritage Foundation, alisema kesi zilizofunguliwa na Republikan zinataka tu sheria zifuatwe.
“Kwa uelewa wangu ni kuwa kesi zilizofunguliwa zinataka tu mahakama kuamuru maafisa wa jimbo kufuata sheria za jimbo,” von Spakovsky alisema.
Democracy Docket inasema Warepublikan wamefungua idadi kubwa ya kesi zinazohusu uchaguzi mwaka huu, nyingi kati ya hizo zikitaka kuwepo kikomo cha idadi ya kura zinazopigwa kwa njia ya posta.
Upigaji kura kwa njia ya posta iliongezeka wakati wa uchaguzi wa rais wa 2020. Lakini majimbo yanayodhibitiwa na Warepublikan tangu wakati huo walipitisha hatua za kuweka ukomo kwa zoezi hilo, wakisema kuwa upigaji kura kwa njia ya posta unapelekea wizi wa kura.
Warepublikan wamepata mafanikio fulani katika kupinga upigaji kura kwa njia ya posta mwaka huu.
Huko Wisconsin, ambako Seneta Mrepublikan Ron Johnson anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa lutein gavana Mdemokrat wa jimbo hilo, mahakama za eneo wiki iliyopita ziliegemea upande wa Warepublikan, na kutoa uamuzi kuwa wafanyakazi wa kaunti hawatakubaliwa kupokea kura zinazotumwa kwa njia ya posta zikiwa na sehemu tu ya anwani za mashahidi.
Huko Pennsylvania, ambako kiti cha Seneti kilichoachwa na Mrepublikan kinagombaniwa, Mahakama ya Juu ya jimbo hilo wiki iliyopita iliidhinisha ombi la Warepublikan kuwa maafisa wa uchaguzi wasihesabu kura zilizotumwa kwa njia ya posta bila ya tarehe au zilizokosewa tarehe.
Lakini huko Michigan, jaji mmoja Jumatatu alitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na mgombea wa Republikan ambaye aliitaka mahakama hiyo kuwataka wapiga kura wote wa Detroit kuwasilisha binafsi kura zao walizopiga au kupiga kura siku ya uchaguzi.
Albert wa Common Cause alisema kesi za hivi sasa juu ya kuhesabu kura za wasiofika kwenye vituo vya kupiga kura bila shaka kuna uwezekano wa kufikia kipindi cha baada ya uchaguzi na kipindi cha uidhinishaji wa kura, ikisababisha kuchelewa kutolewa matokeo ya baadhi ya chaguzi ambazo zitakuwa zina ushindani mkubwa.
“Hususan katika majimbo ambako kura kwa njia ya posta zinaweza kubadilisha matokeo,” Albert alisema. “Tunaendelea kusisitiza kuwa Siku ya Uchaguzi siyo siku ya kutangaza matokeo, na tunaweza kuwa tutasubiri kwa muda kufunga hesabu ya kura.”
Mvutano wa mahakamani baada ya uchaguzi una uwezekano ukahusisha sehemu nyingi za uchaguzi. Zaidi ya kuhesabu na kushughulikia kura zinazotumwa kwa njia ya posta, Democracy Docket inasema inatarajia kuwepo changamoto za kisheria kwa uhalali wa wapiga kura, vitisho dhidi ya wapiga kura na wafanyakazi wa uchaguzi, nadharia za hujuma kuhusu mashine za kupiga kura za kieletroniki na kaunti ambazo zinakataa kuthibitisha matokeo yao ya uchaguzi.