Wapiganaji wa ‘Boko Haram’ wauwa takriban watu 13 Cameroon

Wanajeshi wa Cameroon wakipiga doria Machi 21, 2019, nje ya kijiji cha Mosogo katika mkoa wa Far North wa nchi hiyo ambako wapiganaji wa Boko Haram jihadist wamekuwa wakishambulia tangu owaka 2013.

Wapiganaji wanaoshukiwa kuwa ni wa kikundi cha Waislam wa Boko Haram wamewauwa watu wasiopungua 13 na kuwajeruhi nane wengine katika shambulizi la bomu la mkononi kaskazini mwa Cameroon Jumapili, afisa wa usalama na maafisa wa mji wameiambia Reuters.

Washambuliaji hao ambao hawakutambuliwa walitupa bomu la mkononi katika kundi la watu ndani ya kambi inayowahifadhi watu waliokimbia makazi yao katika kijiji cha Mozogo karibu na mpaka wa Nigeria katika mkoa wa Far North, amesema meya Medjeweh Bouker.

Boukar alifahamishwa na wakazi wa eneo hilo kuwa watu 13 walikufa kutokana na mlipuko wa bomu hilo.

Afisa mmoja wa usalama aliyethibitisha shambulizi hilo kutokea amesema watu wawili waliokuwa wamejeruhiwa pia walifariki, na idadi kufikia watu 15.

Boko Haram imekuwa ikipigana kwa kipindi cha muongo mmoja ili kumtawalisha kiongozi wa dola ya Kiislam nchini Nigeria.

Vita hivyo, ambavyo vimegharimu maisha ya watu 30,000 na kuwakosesha makazi mamilioni zaidi, vimeingia katika nchi ya jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Mwezi Juni 2019, takriban washukiwa wapiganaji wa Boko Haram 300 walivamia kisiwa katika Ziwa Chad huko Cameroon kaskazini na kuuwa watu 24, wakiwemo wanajeshi wa Cameroon waliowekwa katika vituo vidogo vidogo vya kijeshi.