Lori jipya limewasili katika mji wa Sudan Kusini wa Renk, uliojazana na wazee wanaume, wanawake na watoto, nyuso zao zikionyesha uchofu na kiwewe cha safari mbaya na ndefu kutoka kwenye eneo la Sudan lililokumbwa na mapigano.
Watu hao walikuwa miongoni mwa zaidi ya nusu milioni ambao wamevuka mpaka na kuingia Sudan Kusini, ambayo inajitahidi kuwapatia hifadhi watu wanaowasili nchini humo.
Renk iko kiasi cha kilometa 10 kutoka Sudan, ambako mapigano yalizuka mwezi Aprili mwaka jana kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohammed Hamdan Daglo, kamanda kwa kikosi cha RSF.
Tangu wakati huo, vituo viwili vya muda vya Umoja wa Mataifa huko Renk vimeelemewa na mmiminiko mkubwa wa watu wenye khofu, wakikimbia kuokoa maisha yao.