Wafuasi wa waziri mkuu wa zamani aliefungwa jela Imran Khan bungeni walisikika wakilalamikia hatua hiyo, wakidai kuwa kura hiyo iliyopigwa mwezi uliopita iliibwa. Spika wa bunge Ayaz Sadiq amesema kuwa Sharif alipata kura 201 dhidi ya Omar Ayub kutoka kwenye Baraza la Sunni aliejipatia kura 92.
Sharif alihitaji kura 169 ili kujipatia wingi unaohitajika kwenye bunge hilo. Kufuatia siku kadhaa za mashauriano, chama cha Sharif cha Pakistan Muslim League, pamoja na washirika wake, walitengeneza muungano baada ya kura ya Februari 8, ambayo matokeo yake yalicheleweshwa kutokana na kukatika kwa huduma za simu kote nchini.
Serikali baadaye ilisema kwamba kukatizwa kwa huduma hizo kulikuwa muhimu, ili kuzuia mashambulizi dhidi ya wagombea pamoja na vikosi vya usalama. Hata hivyo kucheleweshwa huko kulizua malalamishi kutoka chama cha Khan, kinachosisitiza kuwa uchaguzi huo uliibwa, ili kukizuia kupata wingi wa viti.