Wanajeshi wa serikali walokuwa wamekaribia ngome kuu ya mashariki ya waasi katika mji wa Benghazi walilazimika kurudi nyuma baada ya mashambulio makali ya makombora kutoka majeshi ya Marekani na washirika wa NATO.
Baada ya mashambulio hayo ya Jumamosi na Jumapili makundi ya waasi yalikuwa yanajipanga upya Jumatatu na kuanza kurudisha nyuma majeshi ya serikali yaliyoharibiwa vibaya vifaa vyao na vituo vya kijeshi.
Wapiganaji wa upinzani wanaripotiwa kusogelea mji muhimu wa Adjabiya, lakini maafisa wa upinzani wanasema majeshi ya serikali yanaendelea kuuzingira mji wa magharibi wa Mosrata. Inaripotiwa wanawatumia raia kama kinga dhidi ya mashambulio yeyote ya kigeni, hata hivyo hakuna habari huru za kuthibitisha ripoti hizo.
Katika mji mkuu wa Tripoli maafisa na wanajeshi wa kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi walikuwawanakaguwa majengo yaliyoharibiwa hasa uwanja wa Bab al Aziziya nyumbani kwake kiongozi huyo.