Maafisa wa serikali wanasema hali ilirudi shuri kufikia mchana wa leo baada ya kuimarisha usalama kwenye ofisi hizo za nje za kigeni, baada ya maandamano na ghasia za siku tatu.
Waandamanaji wanashutumu nchi za Magharibi kwa kuisaidia nchi jirani ya Rwanda ambayo inalaumiwa kwa kusaidia uasi unaoongozwa na kundi la M23 la watutsi mashariki ya nchi.
Kundi hilo linaripotiwa kufikia karibu kilomita 5 kutoka mji muhimu wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, kufuatia mapigano yanayozidi kuongezeka .
Rwanda imekanusha tuhuma hizo. Hata hivyo, Congo, pamoja na serikali za Magharibi ikiwemo Marekani na Ubelgiji na taarifa kutoka kundi la kitalaamu la Umoja wa Mataifa zilionyesha kuwa kundi hilo la uasi linanufaika kutokana na msaada wa Rwanda.