Viongozi wa dunia waendelea kutuma salamu za rambirambi kumuenzi hayati Mikhail Gorbachev

FILE -Hayati Rais wa zamani Mikhail Gorbachev

Rambirambi zinaendelea kutolewa kutoka kote ulimwenguni kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Umoja  wa Sovieti Mikhail Gorbachev.

Mikhail Gorbachev alifariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 91, anakumbukwa kama mwanasiasa wa aina yake ambaye aliiongoza nchi yake kuelekea demokrasia.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema katika taarifa kwamba Gorbachev alikuwa mtu mwenye maono mahiri. Alisema kama kiongozi wa USSR, alifanya kazi na Rais wa Marekani Ronald Reagan kupunguza silaha za nyuklia za nchi zote mbili.

Rais Joe Biden

Gorbachev alisaidia kuondoa maelfu ya silaha ambazo ziliitishia Ulaya kwa kutia saini makubaliano ya kikosi cha nyuklia cha masafa ya kati (INF) na Reagan mwaka 1987.

Mnamo 1989, Gorbachev alimaliza vita vya Soviet nchini Afghanistan, vilivyoanza miaka 10 nyuma chini ya Leonid Brezhnev.

Mweka hazina wa Australia alimwita Gorbachev kuwa mmoja wa "viongozi mashuhuri sana ulimwenguni."

Jim Chalmers, Mweka Hazina wa Australia anaeleza: "Pazia limefungwa kwa mmoja wa viongozi muhimu sana ulimwenguni. Alikuwa mtu muhimu wakati wa mambo makubwa. Wakati ulimwengu uliposhuhudia migogoro na mkwamo, aliona amani na uwezekano.

Alikuwa kielelezo cha ujasiri na maono, alikuwa ukumbusho kwamba inahitaji ujasiri zaidi kumaliza vita kuliko kuanzisha. Hakuna historia ya karne ya 20 bila yeye kuchukua jukumu kuu ndani yake. Kwa hiyo, dunia inaomboleza kifo chake leo.”

Rais wa Russia Vladimir Putin alitoa "rambi rambi zake," kulingana na msemaji wa Kremlin.

FILE PHOTO: Rais Vladimir Putin

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema amehuzunishwa sana kusikia kifo cha Mikhail Gorbachev, akimtaja kama "mwanasiasa mkarimu ambaye alibadilisha mkondo wa historia."

Labda muhimu zaidi yalikuwa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya Gorbachev kwa mfumo wa Soviet unaojulikana kama "perestroika" ambao ulifungua njia ya kuvunjika kwa Umoja wa Sovieti na mwisho wa Vita Baridi. Juhudi za kidiplomasia za Gorbachev zilimletea Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1990.

Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza alisema: "Siku zote nilivutiwa na ujasiri na uadilifu alioonyesha katika kumaliza vita baridi kuelekea kwenye amani. ... Katika wakati huu wa uchokozi wa Putin nchini Ukraine, kujitolea kwake bila kuchoka kufungua jamii ya Sovieti bado ni mfano kwetu sote.”

Waziri Mkuu Boris Johnson

Gorbachev ambaye alikuwa mgonjwa alitimiza umri wa miaka 91 wiki moja baada ya uvamizi wa Russia nchini Ukraine mwezi Februari, akiacha kwa kiasi kikubwa mafanikio yake yajieleze yenyewe.