Upinzani wapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020

Tundu Lissu, mgombea kiti cha rais Tanzania

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania ikiendelea kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano, Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,Tundu Lissu, ametangaza kutoyakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu huku Mgombea Urais wa Zanzibar Seif Sharif Hamad akikamatwa kwa kuongoza maandamano visiwani humo.

Siku moja baada ya upigaji kura nchini Tanzania matokeo ya uchaguzi kutoka majimbo na mikoa mbalimbali yameanza kutolewa ambapo Chama cha Mapinduzi kinatangazwa mshindi katika majimbo mengi yakiwemo yaliyokuwa yakishikiliwa na Upinzani.

Hata hivyo wakati matokeo yakiendelea kutolewa, baadhi ya vyama vya Upinzani vimetangaza kutokubaliana na matokeo hayo.

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Tundu Lissu amesema Uchaguzi uligubikwa na kasoro nyingi zikiwemo mawakala wao katika baadhi ya vituo kuzuiwa, ukamataji kura feki na ukiukwaji sheri na taratibu za uchaguzi zinakosesha uhalali wa uchaguzi huu na kutaka Jumuiya za Kimataifa kuingilia kati.

Your browser doesn’t support HTML5

Mahojiano na Iddy Uweso juu ya matokeo ya Uchaguzi Tanzania

Huko visiwani Zanzibar Jeshi la Polisi limemkamata Mgombea Urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo Seif Sharif Hamad na viongozi Wakuu wa chama hicho kwa tuhuma za kuchochea vurugu.

Seif Sharif Hamad kkongozi wa upinzani Zanzibar azungumza na wanahabari

Kukamatwa kwa viongozi kunafuatia kauli ya Maalim Seif kutangaza kupinga matokeo ya Uchaguzi visiwani humo. Kabla ya kukamatwa Seif Hamad alifanya mazungumzo na wanahabari na kuelezea msimamo wao.

Siku ya Jumatano Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Semistocles Kaijage katika mazungumzo na wanahabari ameeleza kuwa tume bado inaendelea kukusanya taarifa zaidi kuhusu mchakato wa Uchaguzi.

Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa na jumuiya mbalimbali za kimataifa ni ripoti za waangalizi wa Uchaguzi huu ambapo taarifa zinaeleza kuwa zitaanza kutolewa kuanzia Ijumaa.

Your browser doesn’t support HTML5

Rashid Ali mwandishi habari azungumzia upinzani kuitisha maandamano

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Idd Uwesu, Tanzania.