“Ndani ya wiki mbili zilizopita, zaidi ya watu 1,000 wameuwawa huku wengine zaidi ya 6,000 wakijeruhiwa na wengine milioni kuathirika moja kwa moja au kukoseshwa makazi tangu Okotoba 2023, “amesema Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya kuratibu masuala ya wakimbizi ya UN, OCHA, pale alipokuwa akizungumza na wanahabari mjini Geneva.
“Ningependa kuongeza kusema kuwa saa chache zilizopita, tumepata ripoti za kuanza kwa mashambulizi ya ardhini kutoka Israel kusini mwa Labanon,” amesema Laerke. Amesema kuwa tayari UN pamoja na mashirika yasio ya kiserikali wameanza kutoa misaada ya chakula , na lishe bora kwa watoto, maji pamoja na misaada mingine ya msingi kwa waathirika.
Jumanne Israel imeanzisha mashambulizi dhidi ya kundi la Hezbollah kusini mwa Labanon, ikieleza kuwa operesheni ya muda inayolenga mahala fulani. Israel imesema kuwa mashambulizi yake yataendelea hadi pale Hezbollah itakapositisha kurusha roketi ndani ya Israel, na pale ambapo hali itakuwa salama kwa familia zinazoishi karibu na mpaka wa Lebanon kurejea makwao.