Serikali hiyo ya mpito itasimamia nchi hiyo iliyoharibiwa na vita kufanya uchaguzi mwisho wa mwaka 2021.
Mazungumzo ya Geneva, yaliojikita katika utaratibu wa Baraza la Mdahalo wa Kisiasa la Libya, umekuwa ukifanyika huku kukiwa na msukumo mkubwa wa kimataifa wa kufikiwa makubaliano ya amani katika vita vya wenye kwa wenyewe Libya. Juhudi za kidiplomasia za miaka iliyopita hazikufanikiwa.
Kaimu mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Stephanie Williams ameuambia mkutano wa waandishi wa habari, Geneva, kuwa wajumbe wa kamati ya ushauri “wametekeleza majukumu yao kwa nia ya kujenga taifa, kwa juhudi za ushirikiano na uzalendo wa hali ya juu.”
Kamati hiyo ya wajumbe 18 imependekeza kuwa baraza la uchaguzi la kila mkoa limchague mwakilishi atakaye wakilisha katika baraza la urais lenye wajumbe watatu, Williams ameeleza.
Waziri mkuu atachaguliwa na jopo la wajumbe 75. Mgombea wa nafasi hiyo atakaye shinda ni lazima apate asilimia 70 za kura zote.
Williams amesema kuwa jopo hilo litatumia orodha iliyotayarishwa kutoka katika mikoa mitatu ya Libya, na kila orodha itakuwa na majina manne, watakao pendekezwa kugombea nafasi ya baraza la urais na nafasi ya waziri mkuu.
Mwanadiplomasia huyo amesema orodha lazima iidhinishwe na watu 17 : wanane kutoka mkoa wa magharibi, sita kutoka mkoa wa mashariki na watatu kutoka mkoa wa kusini ya Libya. Orodha itakayo shinda lazima ipate asilimia 60 ya kura za jopo la wajumbe 75 katika duru ya kwanza. Kurejewa kupigwa kura kunatarajiwa iwapo orodha zote hizo hazijapata kura zinazo takikana, ameongeza mwakilishi huyo.
Williams amesema jopo hilo litapiga kura kupitisha muundo huo uliopendekezwa Jumatatu na matokeo yanatarajiwa kupatikana siku inayofuatia.
Serikali hiyo ya mpito itakuwa “ni uongozi wa muda wa pamoja unaojumuisha wazalendo wa Libya wanaotaka kusaidiana katika kutekeleza majukumu kuliko kugawa nchi yao,” kaimu mwakilishi wa UN amesema.
Marekani imekaribisha makubaliano hayo na kuzisihi pande zote husika nchi Libya “kufanya kazi katika hali ya dharura na nia njema” ili kuweka serikali ya mpito, kulingana na tamko la Ubalozi wa Marekani Libya.
“Ni wakati mwaafaka kusahau mgogoro uliokwisha pita na ufisadi ulioendeshwa na kikundi kidogo kilichokuwa madarakani,” limesema tamko hilo.
Jopo hilo ni sehemu ya juhudi za Umoja wa Mataifa kumaliza ghasia zilizo ikumba nchi hiyo ya Afrika Kaskazini yenye utajiri wa mafuta baada ya kiongozi wake Moammar Gadhafi kupinduliwa mwaka 2011.
Jopo hlo lilifikia makubaliano mwaka 2020 kufanya uchaguzi wa rais na wa bunge ifikapo Disemba 24, 2021.
Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta hivi sasa imegawanyika sehemu ya mashariki na magharibi kati ya utawala wa mahasimu wawili, wote wakiwa wanasaidiwa na makundi ya wanamgambo na mataifa ya kigeni.
Pande hizo zenye kupigana zilikubaliana kusitisha mapigano chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa mwezi Octoba huko Geneva, ikiwemo kuondoka kwa majeshi ya kigeni na mamluki nchini Libya katika kipindi cha miezi mitatu.
Hakuna hatua iliyotangazwa kuhusu suala la wanajeshi wa kigeni na mamluki tangu waliposaini makubaliano ya amani takriban miezi miwili sasa.