UN yataka ubaguzi wa kijinsia kutambuliwa kama uhalifu wa kibinadamu

Wanawake wa Afghanistan.

Jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua rasmi "ubaguzi wa kijinsia" kama uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kuangazia ukandamizaji mbaya wa wanawake na wasichana chini ya tawala kama vile Taliban, nchini Afghanistan.

Kundi la wataalam watano kutoka Marekani, China, Italia, Uganda na Serbia, wanaoshirikiana na shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, wanasema utambuzi huu tayari umepitwa na wakati.

"Ubaguzi wa kijinsia sio tu uwezekano wa kinadharia au maneno tu ya kisheria, lakini ni tishio la kweli, na ukweli unaoendela kushuhudiwa na mamilioni ya wanawake na wasichana ulimwenguni kote - ukweli ambao kwa sasa haujaainishwa wazi katika sheria za kimataifa," wataalam walisema katika taarifa kwenye Umoja wa Mataifa Jumanne.

Wakiangazia Afghanistan kama mfano halisi, wataalam wanadai serikali ya Taliban imeanzisha mfumo wa "ubaguzi, na utawala kandamizi" unaozingatia jinsia.

Tangu kunyakua mamlaka, Taliban wamewazuia wanawake na wasichana kupata elimu ya sekondari, kufanya kazi mbalimbali, kushiriki shughuli nyingi za burudani na kusafiri bila kuandamana na wanaume, kwa mwendo mrefu.