UN: Somalia kuwasilisha maombi ya msaada zaidi wa kimataifa kukabiliana na wanamgambo wa al-Shabab

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre akihutubia Jukwaa la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa Sept. 18, 2023.

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre alisema Alhamisi kuwa serikali yake inaomba msaada zaidi wa kimataifa katika vita vyake vya muda mrefu dhidi ya wanamgambo  wa al-Shabab.

Katika mahojiano maalum na VOA, Barre anasema atafikisha maombi yake kwa Baraza Kuu la UN mwishoni mwa wiki hii kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa vya marufuku ya silaha.

Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre akihojiwa na mwandishi wa VOA Asha Ibrahim Aden, Sept. 21, 2023, mjini New York.

Amesema kuondolewa vikwazo kutaifanya Somalia iwe na uwezo wa kulitokomeza kundi la al-Shabab, ambalo UN na Marekani wameliorodhesha kundi hilo ni taasisi ya kigaidi ambayo inapigana na serikali ya Somalia kwa miaka 16.

Barre alisema kipaumbele cha kwanza kwa Somalia ni usalama, ambao amesema hauwezi kupatikana kikamilifu bila ya jeshi la taifa lililopatiwa mafunzo mazuri na vifaa bora.

“Tunahitaji na tutaiomba jumuiya ya kimataifa waondoe kabisa marufuku ya silaha ambayo iliwekwa kwa Somalia tangu 1992,” alisema.

“Kwa kufanya hivyo, majeshi yetu ya usalama yatakuwa na uwezo wa kuchukua udhibiti kamili na jukumu la usalama wa nchi hiyo.”

Marufuku hiyo iliwekwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 nwakati wa vita vya vya wenye kwa wenyewe.

Imetayarishwa na mwandishi wa VOA Asha Ibrahim, Marekani.