Ukraine: Zoezi la uokoaji laendelea kufuatia shambulizi la Russia lililoangusha majengo kadhaa yaliouwa watu 7

Athari za shambulizi la makombora ya Russia katika mji wa Pokrovsk, Ukraine.

Timu ya uokoaji katika mji wa mashariki mwa Ukraine wa Pokrovsk wanachimba vifusi vya majengo kadhaa yaliharibiwa  na  mashambulizi mawili mfululizo ya makombora yaliyofanywa na Russia Jumatatu ambayo yaliuwa watu wasiopungua saba.

Pokrovsk iko katika mkoa wa Donetsk, ambao umekuwa ni eneo la baadhi ya mapigano makali tangu Russia ilipoanzisha uvamizi wake mwezi Februari 2022.

Pavlo Kyrylenko, gavana wa Donetsk, anasema makombora hayo mawili yalishambulia kwa kupishana kwa dakika 40, na kubomoa majengo ya makazi ya watu, migahawa, maduka na majengo ya serikali na hoteli ambayo ni maarufu kwa waandishi wa habari wa kimataifa.

Athari za mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Russia katika mji wa Pokrovsk, Ukraine.

Waliokufa ni pamoja na mfanyakazi wa dharura katika serikali ya mkoa wa Donetsk.

Wakati huo huo watu wawili waliuawa na makombora yaliyopigwa na jeshi la Russia katika kijiji cha Kruhliakivka kwenye wilaya ya Kupiansk, kulingana na Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.