Uongozi wa kijeshi wa mkoa wa Zaporizhzhia ulisema kupitia ujumbe wa Telegram kuwa kulingana na ripoti mbalimbali za awali, makombora hayo yameharibu duka na kumjeruhi mtu mmoja.
Jeshi la Ukraine pia lilisema Jumanne mifumo yake ya ulinzi wa anga iliangusha droni ya Russia iliyokuwa inashambulia.
Huko Brussels, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema Jumanne kumekuwa na mapigano makali katika maeneo ya mstari wa mbele huko Ukraine, huku wimbi la droni za Russia likifanya mashambulizi dhidi ya miji ya Ukraine.
Stoltenberg alisema kuwa wakati maeneo ya mstari wa mbele huko Ukraine hayajapiga hatua sana katika kipindi cha mwaka uliopita, majeshi ya Ukraine yamesababisha hasara kubwa kwa jeshi la Russia.
Akizungumza kabla ya mkutano wa siku mbili utakao washirikisha mawaziri wa mambo ya nje, Stoltenberg amewataka washirika wa NATO kuendelea kuipa msaada Ukraine.
Alisema kadiri Ukraine itakavyo kuwa na nguvu zaidi katika medani ya vita, ndivyo itakavyo kuwa na sauti zaidi katika meza ya mazungumzo watakapokutana na Russia.
Baadhi ya taarifa katika habari hii zinatokana na mashirika ya habari ya The Associated Press, Agence France-Presse na Reuters.