Uganda yakosolewa katika hatua mpya ya mitandao ya kijamii

Watetezi wa haki za binadamu, wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na viongozi mbalimbali wamekosoa agizo la tume ya mawasiliano nchini humo kutaka mitando yote ya kijamii inayotumika kusambaza habari na maudhui kusajiliwa.

Ilani hiyo iliyotolewa Septemba 7, inataka kila mtu anayetumia mitandao ya kijamii kupeperusha habari, video au biashara kupata idhini ya tume ya mawasiliano nchini Uganda (UCC), amri ambayo itaanza kutekelezwa Oktoba 5.

Tume ya mawasiliano inanukuu ibara ya 27 ya sheria za mawasiliano za mwaka 2013, inayozuia upeperushaji wa maudhui bila kupata leseni.

Amnesty International yakosoa UCC

Shirika la Amnesty International limekemea hatua ya UCC, likisema kwamba ni pigo kubwa kwa uhuru wa kujieleza wakati nchi hiyo inaelekea katika uchaguzi mkuu wa mapema mwaka ujao.

FILE - Waandishi wa Habari na wanachama wa mtandao wa Haki za Binadamu Uganda wakipambana na polisi wakati wa maandamano Kampala, Uganda, May 28, 2013.

Taarifa ya Amnesty International inasema kwamba “hatua ya UCC inarudisha nyuma juhudi zote zilizofanywa Uganda kuhusu uhuru wa kujieleza na kupata habari.” Taarifa hiyo imeongeza kusema kwamba “uhuru wa kujieleza hauhitaji leseni kabisa”, ikiongezea kwamba “UCC inastahili kutambua kwamba uhuru wa kiraia, kisiasa na demkorasia ni sehemu muhimu ya maendeleo.”

Amri ya UCC inakuja wakati serikali ya rais Yoweri Museveni imepiga marufuku mikusanyiko ya watu katika mikutano ya kampeni kutokana na janga la virusi vya Corona, na kutaka wanasiasa kufanya kampeni kupitia mitando ya kijamii, radio, televisheni na kwenye magazeti

Serikali ya Uganda iliweka ushuru kwa watumizi wa mitandao ya kijamii katika hatua iliyosema itapata pesa nyingi kutokana na kile ilitaja kama udaku unaoenezwa kwenye kurasa za Whatsapp, Facebook, Twitter, Skype na Viber.

Wachambuzi wa siasa za Uganda kama Nabende Wamoto, wanasema hatua ya UCC ina lengo la kisiasa lililofichwa, akidai kwamba “inamlenga” mwanasiasa Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi wine, mwenye wafuasi wengi kwenye mitandao tofauti ya kijamii.

Robert Kyagulanyi akosoa UCC

Mbunge wa Kyadongo Mashariki na mwanamziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ambaye ana wafuasi wengi kwenye ukurasa wake wa Facebook, na anayetumia ukurasa huo kufanya kampeni za urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2021, amedai kwamba masharti ya UCC yanamlenga na kundi lake.

Bobi Wine, ambaye wachambuzi wengi wa siasa nchini Uganda wanasema ni mpinzani mkubwa wa rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwakani, amefungua televisheni kwenye mtandao wa Youtube na Facebook, wenye wafuasi wengi.

“Wameeka masharti hayo kwa sababu wanajua kwamba tumefungua televisheni kwenye mtandao kwa jina Ghetto TV, yenye wafuasi wengi. Wanaogopa kwamba tunafikia watu wengi kila saa na kuwasilisha ujumbe wetu kwa wapiga kura, baada ya kutuwekea masharti magumu kuhojiwa kwenye televisheni za kawaida,” amesema Bobi Wine.

Onyesho la Muziki lakushinikiza kuachiwa Bobi Wine Nairobi Kenya.

UCC yatoa ufafanuzi zaidi

Katika ujumbe mfupi wa Twitter, UCC imejibu shutuma kwa kusema kwamba “lengo kuu ni kuwajibisha kila mtu anayeweka maudhui kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, jinsi ilivyo katika vyombo vya habari vya kawaida.”

Wamiliki wa mitandao hiyo wanastahili kutoa habari kuhusu mahali wanapatikana, ushirikiano wa umiliki kama upo, wafadhili na kadhalika.

Mkurugenzi wa tume ya mawasiliano UCC Irene Kaggwa Sewankambo, ameandika ujumbe wa twitter kwamba hatua hiyo sio mpya na kwamba ilianzishwa mwaka 2018 baada ya ushauriano na kampuni zinazotumia mitandao ya kijamii kupeperusha habari, kama vituo vya televisheni na radio, na kuongezea kwamba “kampuni 48 zimesajiliwa kufikia sasa.”

Kila anaotuma maombi ya kusajiliwa anatakiwa kulipa shilingi 100,000 (dola 27).

Muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari unataka maelezo zaidi

Lakini muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari Uganda kupitia kwa katibu wake mkuu Joseph Bagaya, umesema hautatekeleza agizo hilo la UCC, hadi mamlaka hiyo itakapotoa maelezo zaidi kuhusu lengo lake.

‘Kuna vitu vingi sana ambavyo UCC inastahili kutueleza vizuri. Tunakubali kwamba sekta yoyote inastahili kuongozwa na sheria fulani, lakini sheria hizo hazistahili kukandamiza sekta hiyo. Zinastahili kuimarisha ukuaji wake.”

Kulingana na Robert Sempala, mwenyekiti wa muungano wa kutetea haki za waandishi wa habari nchini Uganda, amri ya UCC itaathiri uhuru wa vyombo vya habari.

“Japo UCC ina haki kisheria kusimamia ubora wa habari na maudhui yanayosambazwa ndani ya Uganda kwenye mitandao ya kijamii, hatua ya sasa ina nia mbaya, na inakuja kwa wakati mbaya ambayo nchi inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu, huku tukiwa katikati ya janga la virusi vya corona ambapo wanasiasa wanategemea mitandao ya kijamii kuwasiliana na wapiga kura, huu ni mwendelezo wa sera mbovu za UCC ambazo nia yake ni kubana uhuru wa kujieleza kwa maslahi ya kisiasa.” Amesema Sempala.

Naye John Baptist Imokola, mhadhiri wa habari na mawasiliano katika chuo kikuu cha Makerere amesema “Hii ni sera ambayo lengo lake ni kubana uhuru wa kujieleza na kupata habari. Watu wanatumia mitandao ya kijamii kujieleza kwa urahisi na hata kukosoa serikali. Lengo ni kuwanyamazisha.”

Imokola ameendelea kusema kwamba “UCC haijaeleza namna itakavyotekeleza agizo lake kwa sababu hakuna sheria kufanikisha azimio la tume hiyo, wala tume yenyewe haina vifaa vya kufunga kurasa za mitandao ya kijamii zinazopeperusha maudhui.”

Hisia za raia wa kawaida

Wasiwasi kati ya raia wa kawaida wa Uganda ni namna UCC itakavyowajibisha watumiaji wa mitandao hiyo wanaosambaza maudhui, sauti au video wanazopokea kwenye mitandao. Kwenye mitandao ya kijamii wengi wanakashifu agizo la UCC na kuuliza iwapo video imesambazwa na watu 1000 kwa mfano, wa kwanza kuisambaza ndiye atakayewajibishwa au ni kila mtu aliyesambaza video hiyo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC.