Tume ya taifa ya uchaguzi ilimtangaza Rais Yoweri Museveni kuwa mshindi kwa awamu ya sita kwa kupata asilimia 58 ya kura.
Lakini Robert Kyagulanyi, mwanasiasa, mwanamuziki na mgombea mkuu wa upinzani – maarufu katika fani ya muziki kwa jina la Bobi Wine – alisema kura zilikuwa na kasoro na kutokana na manyanyaso waliyofanyiwa wafuasi wake na kujazwa kura bandia katika sanduku la kura.
Wagombea kadhaa wa upinzani wanakubaliana na Wine kuhusu hilo na wanataka taifa kuikataa serikali ya Museveni.
Wine aliwekwa kizuizini nyumbani kwa siku 12 baada ya uchaguzi lakini bado aliweza kuhamasisha uungwaji mkono wa kimataifa.
Makundi ya haki za binadamu na serikali za kigeni – ikiwemo Marekani – waliikosoa serikali ya Uganda kwa kuzima intaneti wakati wa uchaguzi na kuwapiga marufuku waangalizi wa uchaguzi kutoka nje.
Seneta wa Marekani Bob Menendez wa New Jersey amesema anapanga kushirikiana na utawala wa Rais Joe Biden kuitaka Uganda iwajibike kutokana na dosari hizo za uchaguzi.
“Kutakuwa na majibu kwa wale wanaoendelea kujihusisha kwa makusudi kukandamiza demokrasia,” alisema.
Pat Thaker, mchambuzi katika kitengo cha intelijensia cha uchumi, kinacho fanya utafiti na uchambuzi cha kampuni ya habari ya Uingereza, Economist Group, amesema serikali ya Museveni ilivuka mipaka kuukandamiza upinzani..
Thaker anaamini huo ni ushahidi kuwa serikali inamuona Wine kama tishio kubwa kwa utawala wa Museveni.
“Ukweli, unaweza kusema [Wine] aligeuza mazingira ya kisiasa kuelemea upande wake na ameanzisha kitu ambacho huwezi kukibadilisha,” Thaker alisema katika mahojiano na VOA. “Amefungua sanduku la matatizo.”