Trump atafakari kutoa katazo jipya la kuingia Marekani

Wahamiaji kutoka Honduras wakiwa wanapumzika katika mji wa Pijijiapan, Mexico kabla ya kuendelea na msafara wao wa kuingia Marekani, Octoba 25, 2018.

Uongozi wa Trump unaripotiwa kuwa unatafakari iwapo utoe amri mpya ya kiutendaji inayolenga kuzuia wanaoomba hifadhi na wahamiaji kutoruhusiwa kuvuka mpaka wa Marekani – Mexico wakati msafara wa wahamiaji ukiendelea kusonga mbele kuelekea kaskazini kupitia Mexico.

Habari zinazo wanukuu maafisa kadhaa wasiotajwa majina zinasema serikali inapima idadi kadhaa ya hatua za kiuongozi na kisheria zinazojikita katika usalama wa taifa kuzuia uwezo wa wahamiaji kuomba hifadhi.

Ingawaje hakuna taarifa za uamuzi uliofikiwa mpaka sasa, mawakili wa uhamiaji wameiambia VOA uamuzi huo mara moja utapingwa kwa kupelekwa mahakamani.

Hata hivyo msafara wa maelfu ya wahamiaji kutoka Amerika ya kati unaendelea na safari kupitia Mexico, wakiwa na matumaini ya kuingia Marekani.

Hadi Ijumaaa wahamiaji hao walikuwa wanapumzika katika mji wa Piji-jiapan nchini Mexico, katika jimbo la mashariki la Chiapas, huku Pentagon ikitarajia kutuma wanajeshi 800 kushika doria kwenye mpaka wa marekani na Mexico.

Rais Donald Trump amesema kwamba wanajeshi wametumwa mpakani kusaidia kukabiliana na hali ya dharura ya kitaifa na kutaka msafara huo wa wahamiaji kurejea wanakotoka.

Wanajeshi wanaotumwa watasaidiana na walinzi wa kitaifa 2000 ambao tayari wanashika doria kwenye mpaka wa marekani na Mexico.