Pia vinakabiliwa na changamoto ya mrundikano wa kodi za usajili huku serikali ikiahidi kuwa mwaka 2023 itasimamia uchumi wa vyombo vya habari pamoja na maslahi ya waandishi.
Mishahara midogo, ukosefu wa bima za afya na pensheni kwa waandishi wa habari vinaripotiwa ni moja ya manung’uniko ya muda mrefu licha ya ahadi kutolewa na watawala wanapo kuwa katika majukwaa ya kisiasa.
Kutoshirikishwa katika mipango endelevu ya taifa imekuwa ni chanzo kwa vyombo vya habari kutokuwa na mapato mazuri hasa kwa vyombo ambavyo vinarusha matangazo yake ndani ya mkoa.
Mmoja wa wadau wa habari na msimamizi wa kituo cha radio cha Hidaya fm Ally Zumo kutoka kigoma anasema juhudi zaidi zinahitajika kwa vyombo vya habari kujikwamua kiuchumi hasa vinapokabiliwa na mrundikano wa kodi
Wadau wa habari wanaeleza maslahi ya waandishi wa habari hayawezi kuimarika ikiwa hali ya uchumi katika vyombo hivyo haijapatiwa ufumbuzi na pia kuna suala jingine la ukosefu wa matangazo ambayo ni moja ya mhimili wa vyombo vya habari kuwa na pato la kuendesha shughuli zake.
Hasani Yusufu msimamizi wa radio Iqra fm ya jijini Mwanza akizungumza na Sauti ya Amerika anasema licha ya kuandika miradi mingi ya kuomba matangazo ili kuendesha radio lakini bado kumekuwa na hali ya kutokuthaminiwa na kujiona kama wanadharaulika ukilinganisha na radio kubwa zenye majina
Hata hivyo waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Mwaka 2023 serikali itaweka nguvu za kutosha kwenye suala la maslahi ya waandishi wa habari na uchumi wa vyombo vya habari ikiwemo mikataba ya wana habari ili kuongeza ari katika utendaji wao.
Ally Zumo anasema waziri Nnape ana kazi kubwa ya kufanya kutekeleza aliyoyaahidi na kuweka matumaini makubwa kwa wanahabari .
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhan