Wamesema serikali imekuwa ikiwataka walime mazao mbadala, lakini imeshindwa kutekeleza wito huo ambao wakulima hao walisema kuwa umetawaliwa na siasa na hauna uhalisia.
Ukosefu wa mikakati madhubuti ya kuwapatia pembejeo na wataalamu watakaowafundisha mbinu za ulimaji mazao mengine ndiyo sababu inayowafanya kuendelea kulima zao hilo mbali na athari mbalimbali ambazo wanazishuhudia.
Akizungumza na Sauti ya Amerika Deo Malechela mkulima wa tumbaku mkoani Tabora alisema serikali imekuwa ikitoa wito kwa wakulima katika ulimaji wa mazao mengine lakini serikali imeshindwa kuwasimamia na kuwapelekea wataalamu.
Malechela alisema ukosefu wa maelekezo ya kitaalamu kumewafanya wakulima kuendelea na kilimo cha tumbaku ambacho kimekuwa kikiharibu mazingira na kuufanya mkoa wa Tabora kuwa jangwa kutokana na ukataji miti.
“Tumekuwa tukihamasishwa kulima alizeti, shida kubwa, hili zao limeshikiliwa na wanasiasa ambao wamekuwa wakija kuhamasisha kwamba tulime alizeti na kama unavyojua katika mkoa wa Tabora alizeti ni zao jipya lakini tumekuwa hatupewi ule utaalamu. Watu wengi wanaitikia kwenye zao hilo lakini wamekuwa wakipungukiwa utaalamu.” alisema Malechela.
Waziri kivuli wa kilimo maendeleo ya mifugo na uvuvi katika serikali kivuli ya ACT Wazalendo Mtutura Abdallah alisema serikali inatakiwa kuwajibika kwa kuwapatia wakulima mbegu bora na mikopo ili waweze kuachana na kilimo cha tumbaku.
Kwa kuongezea wakulima wanaweza kuingia katika kilimo cha mazao kama vile korosho, alizeti na matunda, lakini wanahitaji msaada mkubwa ili wafike sehemu ambayo wataona manufaa ya mazao hayo, na hiyo ndiyo njia ya kuwafanya waachane kilimo cha tumbaku ambacho kimekuwa siyo rafiki kwa mazingira.
Alisema “Kwahiyo inachotakiwa serikali kufanya ni kuwahimiza wananchi wale wajikite zaidi kulima mazao haya ambayo hayana athari lakini vilevile ni rafiki kwa mazingira” aliongeza kuwa kusema “na wakinufaika na mazao hayo ninaamini wataachana na zao la tumbaku kwanza zao la tumbaku linauharibifu mkubwa sana wa mazingira.”
Nao wataalamu wa afya walieelezea athari ya matumizi ya tumbaku wakisisitiza zao hilo linaweza kusababisha magonjwa ya moyo, saratani, magonjwa ya kupumua, na hata kupunguza umri wa kuishi kwa mtumiaji.
Daktari wa afya ya akili na saikolojia Rajabu Mabruki anasisitiza kuwepo kwa elimu ya kutosha na pia ziwekwe mbinu mbadala za upatikanaji wa ajira zitakazowaokoa wakulima na watumiaji wa tumbaku.
“Siamini kwamba asilimia 90 ya ajira katika nchi zetu za Afrika Mashariki inazalishwa na tumbaku, tunaweza tukafanya ajira nyingine mbadala kimsingi tuendelee kupeana elimu na tuisisitize serikali itoe elimu kwa jamii juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku.” Alisema Daktari huyo.
Tunahitaji chakula, sio tumbaku ni kauli mbiu iliyobeba maadhimisho ya mwaka huu ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa uzalishaji mazao mbadala na kuwahimiza wakulima kulima mazao endelevu na yenye lishe, hali ambayo itawafanya wakulima kuitaka serikali kuongeza nguvu katika kulitokomeza zao hilo.
Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.