Hatua hii ilichukuliwa baada ya wabunge hao kuchukua uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya chama hicho kuwapitisha.
Chadema imesema Jumatatu Baraza Kuu la chama litasikiliza rufaa zilizowasilishwa na wabunge hao ambao wamefutwa uanachama.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje, John Mrema.
“Walikuwa wanachama wetu 19 ambao walishafukuzwa na kamati kuu, walikata rufaa kwenye baraza kuu. Tumewapelekea barua rasmi za kuwaita kwa ajili ya kusikiliza rufaa zao.”
Wabunge ambao rufaa zao zitasikilizwa ni pamoja na Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Hata hivyo wabunge hao wanawake wamekataa kuzungumzia suala hilo.
Novemba mwaka 2020 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uamuzi wakuwavua uanachama wabunge hao 19 wakati akisoma maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichokaa kuwajadili wabunge hao.
Hatima ya wabunge hao wanawake itajulikana rasmi Jumatano baada ya rufaa yao kusikilizwa na kutolewa maamuzi, endapo baraza kuu litakubaliana na hatua ya kuwavua uanachama, haijulikani kama wabunge hao watachukua hatua gani za ziada.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.