Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 09:26

CHADEMA yagoma kushiriki kongamano mpaka suala la katiba lipewe kipaumbele


Freeman Mbowe (Picha na Michuzi Blog).
Freeman Mbowe (Picha na Michuzi Blog).

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ndio chama kikuu cha upinzani, Tanzania, kimesema hakitashiriki katika mkutano na kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wiki ijayo.

Akizungumza Ijumaa Jjijini Dar es Salaam na waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichofanyika Jumatano Machi 16, 2022, jijini humo, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema watashiriki pale kituo hicho kitakapokubaliana na Chadema juu ya kuanza kuweka kipaumbele cha katiba mpya badala ya mambo mengine.

Mbowe amesema wao kama chama hayo maridhiano yanayozungumzwa kupitia TCD hawajashiriki kuyaandaa na hata viongozi wao walipotafuta taarifa za kina hawakuona njia nzuri kuhusu katiba mpya.

“Tumeangalia na kamati kuu nia gani iko nyuma ya TCD na hoja zake hatuoni ufumbuzi wa kuipata katiba ya nchi yetu, tunaona mkakati wa kuakhirisha ajenda ya katiba kwa taifa hili na sisi hatuwezi kuwa sehemu ya hilo,”amesema Mbowe.

Aidha ameongeza kuwa “Sio Mbowe wala kiongozi yeyote wa Chadema atashiriki vikao hivyo, japo nimesema tutashiriki kwenye mazungumzo na yeyote mwenye nia ya katiba mpya kwanza”.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Chadema ameweka wazi mambo aliyozungumza na Rais Samia Suluhu Hassan hapo Machi 4, 2022 saa kadhaa baada ya kuachiwa na mahakama kwenye kesi ya ugaidi iliiyokuwa inamkabili.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

Amesema alipokwenda kuzungumza na Rais, mengi yaliongelewa, yeye alinyamaza ili akutane na kamati kuu ya chama chake ndipo atakapotoa kauli iwe ya Chama na wala sio ya kwake.

“ Tumekubaliana na Rais kutafuta njia za haki za mazungumzo na mashauriano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu,” alisema Mbowe.

“Pia tulikubaliana kuwa tuna tatizo kubwa la kutokuaminiana, kwa sababu tumekuwa na urafiki wa mashaka na tukakubaliana ili kuvuka kikwazo hicho lazima kila upande ujaribu kujenga imani kwa mwenzake na majibu yatapatikana.”

Hata hivyo ameongeza kuwa “aache kuzungumzia neno amani na azungumze neno haki na yeye (Rais) au mtu mwingine atambue kwamba Chadema ni chama kikuu cha upinzani kamwe huwezi kukiacha nje ”.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhan, Tanzania

XS
SM
MD
LG