Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani kuanzisha uchunguzi wa kutokuwa na imani na Rais Biden

Spika wa Bunge la Marekani Kevin McCathy.

Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Kevin McCathy amesema kwamba anaanzisha uchunguzi akiwa na nia ya kupitisha mswada wa kutokuwa na Imani na rais Joe Biden.

Hatua hiyo inaonekana kuchochewa na shinikizo kutoka rais wa zamani Donald Trump na washirika wake, ikiashiria mwaka wa uchaguzi utakaokuwa na mvutano mkubwa.

Kupitia taarifa ya Jumanne, McCathy amesema kwamba uchunguzi wa Bunge kwenye familia ya Biden mwaka huu umefichua “utamaduni wa ufisadi”, unaohitaji kuchunguzwa kwa kina.

“Hizi ni tuhuma za utumizi mbaya wa madaraka, kuzuia uchunguzi pamoja na ufisadi,” amesema McCathy.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ikulu ya Marekani imetaja juhudi hizo kuwa siasa zenye msimamo mbaya zaidi.

"Wabunge wa repablikan wamekuwa wakimchunguza rais kwa miezi 9 bila kupata ushahidi wowote,” amesema msemaji wa Ikulu Ian Smith.

Kufikia leo, hakuna rais wa Marekani aliyewahi kuondolewa kwenye ikulu kupitia kura ya kutokuwa na Imani. Hata hivyo rais Richard Nixon hapo 1974 alijiuzulu wakati bunge lilipokuwa likijiandaa kupiga kura ya kutokuwa na Imani.