Shambulizi la guruneti laua watoto 3 Burundi

Ramani ya Burundi

Watoto wa tatu wameuawa na watu wengine wa nane kujeruhiwa katika shambulizi la guruneti lililotokea Alhamisi asubuhi katika mtaa moja nje ya mji mkuu Bujumbura, gazeti la mtandaoni la SOS media limeripoti.

Shambulizi hilo limefanyika saa tatu asubuhi majira ya Burundi katika mtaa wa Rubirizi, kaskazini mwa nchi hiyo, washambuliaji walilenga nyumba ya kinyozi na duka.

Mashahidi wanasema watoto hao waliofariki walikuwa wanatizama televisheni.

Mkanda wa video uliosambazwa kwenye mtandao ya kijamii -- WhatsApp unaonyesha wengi kati ya waliojeruhiwa ni vijana.

Gazeti hilo limenukuu idara ya polisi Burundi ikithibitisha shambulizi hilo, na kuongeza kuwa washukiwa wa tatu wamekamatwa kwa uchunguzi zaidi.

Hili ni shambulio la kwanza baya kutokea tangu rais mpya Evariste Ndayishimiye achukuwe hatamu za uongozi hapo juni 18 mwaka 2020.