Rusesabagina mwenye umri wa miaka 67 alihukumiwa mwezi Septemba akikabiliwa na mashtaka nane ya ugaidi yanayohusiana na harakati za taasisi inayoupinga utawala wa Rais Paul Kagame na anashikiliwa katika jela nchini Rwanda.
Rusesabagina amekanusha mashtaka yote na kukataa kushiriki katika kesi ambayo yeye na wafuasi wake wamedai ina ushawishi wa kisiasa. Hata hivyo hakuwepo mahakamani mjini Kigali Jumatatu kusikiliza rufaa ambayo ilianza dhidi yake na alichagua kubaki jela.
Mwendesha mashtaka wa umma Jean Pierre Habarurema ameiambia mahakama kwamba hawakubaliani na uamuzi wa kumpatia Rusesabagina kifungo cha miaka 25 badala yake wanataka apewe kifungo cha maisha.
Rusesabagina amekubali kuwa na mchango wa kuongoza kundi la MRCD lakini amekanusha uwajibikaji wa kufanya mashambulizi kutoka kundi jingine lililokuwa na silaha la FLN.