Uamuzi ambao mahakama ya juu nchini Uingereza imesema Rwanda haina mazingira salama ya kuwapokea wahamiaji hao. Uamuzi huu unafuatia rufaa iliyotolewa maamuzi na mahakama kuu nchini Uingereza mwezi Juni mwaka huu kufuatia makubaliano ya serikali za Uingereza na Rwanda kuhusu Rwanda kuwapokea wahamiaji hao.
Hili ni sakata ambalo limedumu kwa muda wa miaka miwili sasa.
Mwezi Juni mahakama hiyo iliweka pingamizi ya kuwapeleka Rwanda wahamiaji hao. Wakati huo pia Mfumo wa sheria na watetezi wa haki za binadamu nchini Uingereza walisema kwamba Rwanda haina mazingira salama ya kuwapokea wahamiaji hao walioingia nchini Uingereza kinyume cha sheria.
Sasa baada ya kutolewa uamuzi huo Jumatano asubuhi, msemaji wa serikali ya Rwanda Bi Yolanda Makolo ametoa tangazo ambalo linalaani uamuzi wa mahakama ya juu ya Uingereza kuhusu Rwanda kutokuwa salama kuwapokea wahamiaji hao.
Msemaji wa serikali amesema ngazi za sheria nchini Uingereza zina mamlaka na haki ya kuamua vyovyote kisheria lakini jambo lisilostahili na lawama zinazohusishwa na uamuzi huo kuhusu Rwanda kutokuwa salama pindi wahamiaji hao wakipelekwa.
Uamuzi wa mahakama ya juu nchini Uingereza umesema kwamba kuna hatari kwamba wahamiaji hao wakipelekwa Rwanda wanaweza kukabiliana na hatari ya kurudishwa katika mataifa yao ya asili walikokimbia suala ambalo ni hatari kwa maisha na usalama wao kwa ujumla.
Lakini kupitia tangazo kwa umma, msemaji wa serikali ya Rwanda Bi Yolande Makolo amesema, siku zote Rwanda imeshirikiana na Uingereza katika kupanga mkakati huu na kwamba Serikali ya Uingereza iliridhia na kuhakikisha kwamba Rwanda ilikuwa salama kwa wahamiaji hao.
Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanalichukulia suala hili kwa mitazamo tofauti,
Serikali ya Rwanda kupitia tangazo la msemaji wake imesema kwamba hadi sasa inaendelea kuwaheshimu wakimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na miongozo ya shirika la Umoja wa Maitaifa linalohudumia wakimbizi UNHCR na kwamba mashirika mbalimbali ya kimataifa yamelihakiki hilo.
Kwa mara ya kwanza mpango wa kuwapeleka Rwanda wahamiaji haramu kutoka Uingereza ulisainiwa kati ya serikali za Rwanda na Uingereza mwezi April mwaka 2022 ambapo Uingereza iliipatia Rwanda kitita cha pauni za Uingereza zaidi ya milioni 120 huku ikitazamiwa wakati huo kila mhamiaji angelipiwa bajeti ya pauni elfu 12.000.
Waziri mkuu wa Uingereza Rish Sunak yeye amesema kwamba mpango wa kuwazuia wahamiaji haramu wanaoingia nchini Uingereza kwa boti bado ni imara.
“Mkakati wangu wa kuwazuia wahamiaji haramu kwa kutumia boti bado ni imara, serikali imekuwa ikijishughulisha na mkataba mpya na Rwanda, na tutaendelea kuukamilisha licha ya uamuzi wa leo, ikilazimika, niko tayari kutazama upya sheria zetu za ndani’’ amesema Sunak waziri mkuu wa Uingereza kupitia mtandao wake wa X zamani ukijulikana kama Twitter.
Rwanda ilitakiwa kuandaa mazingira bora ikiwa ni pamoja na kuwajengea makazi ya kuishi lakini pia kuwapa haki ya kuomba kuishi nchini Rwanda au kuanza mchakato mpya wa kuomba kwenda katika nchi za ulaya na mahali pengine ulimwenguni lakini wakitokea Rwanda.
Lakini tangu wakati huo suala hili limezua utata mkubwa na tayari mawaziri wawili wa mambo ya ndani nchini Uingereza Prit Patel na Suella Bravernman wameenguliwa kwenye nyadhifa zao wengi wakihisi mchakato huu ukiwa ni sababu mojawapo.