Jeshi la anga la Ukraine limesema ulinzi wa anga wa nchi hiyo limeyatungua makombora 10 yaliyorushwa na Russia.
Vifusi vilivyokuwa vinaanguka kutoka kwenye makombora yaliyotunguliwa yameiharibu hospitali ya watoto na mfumo wa maji ya jiji, Meya wa Kyiv, Vitaly Klitschko amesema, wakati Serhiy Popko, mkuu wa utawala wa jeshi la Kyiv amesema mabaki hayo pia yalidondokea nyumba kadhaa.
Russia imethibitisha kwa mara nyingine tena kwamba ni nchi ya kikatili ambayo imefyatua makombora jana usiku na kuyapiga maeneo ya makazi ya watu, shule za chekechea, na mitambo ya nishati wakati huu wa majira wa baridi” alisema Zelenskyy siku ya Jumatano aliandika kwenye mtandao wa kijamii “Kutakuwa na jibu. Bila shaka.”
Zelenskyy aliongeza kuwa yeye na rais wa Marekani Joe Biden wamekubaliana kuongeza idadi ya mfumo wa ulinzi wa anga, na kuwa Russia “imeonyesha umuhimu wa uamuzi huo”.
Utawala wa Biden siku ya Jumanne ulitangaza msaada mpya wa kijeshi wa mpaka dola milioni 200, msaada ambao unajumuisha ulinzi wa anga wa makombora na vifaa kwa Ukraine kutokana na rasilimali ambazo ziliidhinishwa awali.