Ripoti ya Jarida la Wall Street Journal inasema wachunguzi wa Shirika la Afya Duniani -WHO ambao hivi karibuni waliitembelea China ili kujua asili ya kuibuka kwa virusi vya COVID-19 hawatatoa ripoti yao ya awali ya uchunguzi wao kama ilivyoahidiwa.
Maelezo hayo yaliyo chapishwa Alhamisi, yalieleza kuwa timu ya WHO iliamua kutotoa ripoti yake ya awali katikati ya mivutano kati ya Beijing na Washington.
Hata hivyo kundi jingine la wanasayansi wa kimataifa limetoa wito kwa WHO kufanya uchunguzi mpya wa asili ya COVID.
Wanasayansi wanaotoa wito wa uchunguzi huo mpya walisema katika barua ya wazi Alhamisi kwamba timu ya WHO haikuwa na mamlaka, uhuru, au uwezo muhimu wa kufanya uchunguzi kamili na usiozuiliwa.
Wanasayansi hao pia walibainisha katika barua yao kwamba wachunguzi wa WHO nchini China waliungana na wenzao walioko China.