Cyril Ramaphosa alisema amesikitishwa sana na hatua hiyo, ambayo aliitaja kuwa isiyo na msingi, na kutaka marufuku hiyo kuondolewa haraka.
Rais Cyril Ramaphosa ameeleza :"Tunatoa wito kwa nchi hizi ambazo zimeweka marufuku ya kusafiri kwa nchi yetu na nchi nyingine za kusini mwa Afrika kubadili mara moja na kwa haraka maamuzi yao na kuondoa marufuku waliyoweka kabla ya uharibifu wowote zaidi kwa uchumi wetu na kwa maisha ya watu wetu. Hakuna uhalali wa kisayansi wa kuweka masharti haya."
Uingereza, umoja wa Ulaya na Marekani ni miongoni mwa walioweka marufuku ya kusafiri.
Omicron imeainishwa kama aina ya virusi vinavyotia wasiwasi. Ushahidi wa mapema unaonyesha kuwa vina hatari kubwa ya kuambukiza tena.
Virusi hivyo vipya viligunduliwa nchini Afrika Kusini mapema mwezi Novemba na kisha kuripotiwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatano iliyopita.
Aina hiyo imeambukiza kwa wingi katika jimbo lenye watu wengi zaidi la Afrika Kusini, Gauteng, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na sasa vipo katika majimbo mengine yote nchini humo.