Ushindi huo umetokea wakati uchaguzi wa nchi hiyo umeripotiwa kuwa na utata na kusababisha hali ya wasiwasi, wanasiasa wa upinzani wakidai kuwepo na udanganyifu katika kuhesabu kura.
Azali, aliyeingia madarakani mwaka 2016, amepata asilimia 60.77 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa Marchi 24, akifuatiwa na mgombea wa chama cha Juwa katika kinyang'anyiro hicho Mahamoudou Ahamada, aliyepata asilimia 14.62.
Azali, mwenye umri wa miaka 66, atanaza mhula mpya wa miaka mitano katika visiwa vya Comoros, vyenye wakazi 800,000, katika moja ya nchi maskini zaidi duniani na yenye misukosuko ya kisiasa.
Hesabu ya kura ilikabiliwa na vurugu, maafisa wa usalama wakivunja maandamano ya upinzani kwa nguvu zote. Japokuwa Rais Azali anakiri kuwepo dosari, anataka nchi hiyo kuangazia umoja na ujenzi wa taifa.
Azali Assoumani, ameeleza kuwa : "Ni kweli kwamba kulikuwepo makosa lakini tunafuraha kwamba mambo hayakuwa mabaya sana. Tunajipongeza wenyewe, tunamshukuru Mungu na watu wa Comoros. Lakini nilivyosema, yale tumefanya ndio rahisi, wakati mgumu sasa ni kujenga nchi na nahitaji mchango wa kila mtu."
Wanasiasa wa upinzani kama Mugni Baraka, aliyemaliza katika nafasi ya tatu, wanadai kwamba dosari katika hesabu ya kura, zilizoripotiwa na tume ya uchaguzi katika vituo kadhaa siku ya Jumapili, ni sawa na mapinduzi ya serikali na kutaka serikali kukataa matokeo hayo.
Baraka amesema : "Tunachukulia kwamba hakuna uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili. Kilichofanyika kilikuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyopangwa na Azali Assoumani na kundi lake. Jeshi lilishiriki katika mapinduzi hayo kwa sababu tuliona wanajeshi wakibeba masanduku ya kupigia kura katika vituo vingi kama Anjouan na Moheli."
Vyanzo vya habari vya Comoros vimeripoti kuwa watu 12 wamejeruhiwa, wakati polisi walipotumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya wanasiasa na wafuasi wa upinzani, waliokuwa wakiandamana katika mji wa Moroni, wakipinga matokeo ya kura.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC