Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:24

Upinzani hawaamini taarifa za jaribio la kumuua Rais wa Comoro


Upinzani wa Comoros unasisitiza kwamba taarifa ya Ikulu ya Moroni kwamba kulikuwepo na jaribio la kumuua Rais Azali Assoumani akiwa katika kampeni za uchaguzi wa Rais, sio ya kuaminika.

Upinzani wa Comoros hawaamini kulikuwepo na jaribio dhidi ya Azali
please wait

No media source currently available

0:00 0:02:48 0:00

Ikulu ilieleza kwamba kiongozi huyo akiwa katika kisiwa cha Nzwani Alhamisi katika maeneo ya milimani kulikuwepo na mlipuko uliyosababisha majabali kuporomoka wakati msafara wa magari yake ulipokuwa unapita.

Kuna hali ya wasi wasi inayoendelea katika kisiwa cha Nzuwani tangu vitendo vya uasi vilipotokea mwaka 2018, na hali ya kwamba wakazi wengi wa kisiwa hicho wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo uloitishwa mapema na Rais Azali.

Duru ya kwanza ya uchaguzi

Duru ya kwanza ya Uchaguzi huo itafanyika Machi 24, kufuatia kubadilishwa kwa katiba mwaka 2018, ili kuondoa mfumo wa muhula mmoja wa utawala wa Rais.

Houmed Msaide, Meneja wa kampeni za rais azali, anasema mabaki ya baruti yaliyopatikana katika eneo lililotokea mlipuko na kusababisha majabali kuporomoka chini hadi barabarani, sekunde chache tu kabla kuwasili gari la rais.

Hakuna aliyejeruhiwa kutokana na ajali hiyo. Maafisa wa upinzani wanasema tukio hilo ni la kawaida kwani hilo ni eneo ambalo mawe huporomoka mara kwa mara.

Kukosekana upinzani

Hakuna mgombea wa upinzani katika kiti cha urais anayeshiriki katika uchaguzi huo baada ya mahakama kuu ya Comoro kuwaondoa katika kinyang'anyiro hicho kwa sababu za kasoro mbali mbali katika maombi yao.

Katibu wa chama cha upinzani cha Djuwa, Ibrahim Mohamed Soule, amesema timu ya azali hubuni mashambulizi au matukio ya bandia ili kuwapotosha wananchi kwamba upinzani hawataki uchaguzi wa huru.

Muasisi wa Djuwa

Chama hicho cha upinzani muasisi wake ni rais wa zamani aliyeko kizuizini nchini Comoros, Ahmed Abdallah Sambi,

Soule ni miongoni mwa wagombea wawili wakuu wa upinzani walioondolewa na Mahakama Kuu kushiriki katika uchaguzi huo.

Ibrahim Mohamed Soule, Katibu Mkuu wa chama cha Djuwa anaeleza : "Kwanza una muamuzi anaesimamia uchaguzi aliyechaguliwa na mtu mmoja, mtu huyo huyo anayegombania nafasi ya juu. Na una mahakama ambayo hii leo imedhihirisha ina upendeleo kwa kuwaondoa wagombea wawili wa kuaminika na wenye uwezo wa kumshinda mgombea wa serikali.

Wasemavyo wachambuzi

"Kuna wagombea 14 walobaki na 13 kati yao ni wagombea huru, na wachambuzi wanasema hawaamini uchaguzi utakuwa wa huru bila ya kushiriki kwa upinzani."

Mabadiliko ya katiba yatamruhusu hivi sasa Azali kuweza kubaki madarakani kwa mihula miwili ya miaka mitano kila muhula na hivyo kuweza kubaki hadi 2024. Lakini wananchi wa Nzwani wanadai kuwa zamu yao chini ya katiba iliyopita itakuwa 2021, na hivyo hawatambui uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG