Your browser doesn’t support HTML5
Wagombea 12 wa kiti cha rais tangu Jumapili wamewataka wafuasi wao kupinga juhudi za Tume ya Uchaguzi ya Comoros CENI kuwasilisha masanduku ya kura makao makuu yaliyowekwa ndani ya jengo la bunge mjini Moroni.
Baadhi ya viongozi wanaripotiwa wamekamatwa na wagombea wawili wamejeruhiwa na kulazwa hospitali.
Tume ya Uchaguzi haijasema lolote kuhusiana na ghasia hizo na tuhuma za wizi wa kura lakini inatarajiwa kutangaza matokeo ya awali hii leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani
Waziri wa mambo ya ndani Mohamed Daoud maaruf kwa jina la Kiki alizungumza na waandishi wa habari na kukanusha ghasia kutokea akidai wananchi wa Comoro wametekeleza wajibu wao wa kidemokrasia kwa utulivu na amani.
Haijulikani idadi kamili ya waliojeruhiwa kukiwa na habari za takriban watu watano waliouliwa kwenye ghasia za uchaguzi.
Tume ya uchaguzi kwa upande wake imeripotiwa ikiendelea na zoezi la kuhesabu kura zilizokwisha wasili makao makuu katika jengo la Bunge na inatarajiwa kutoa matokeo ya awali Jumatatu jioni.
Vituo vya kupiga
Vituo vya kupiga kura katika wilaya mbali mbali za visiwa hivyo vilifunguliwa bila ya matatizo makubwa na upigaji kura ukaendelea kwa utulivu . Lakini kufikia mchana kulikuwepo na ripoti za ghasia kuzuka katika kiswa cha pili kwa ukubwa cha Nzwani ambako wawakilishi wa wagombea 12 wa kiti cha rais waliripoti kuwepo na sanduku za kura zilizojazwa vyeti vya kura vinavyompendelea Rais Azali.
Ghasia zimeripotiwa pia katika ngome za upinzani katika kisiwa cha Ngazija, kama ilivyoonyeshwa na video katika mitandao wa kijamii na shirika la habari, “Habari za Komoro”.
Baadhi ya wapiga kura walieleza masikitiko yao juu ya jinsi upigaji kura ulivyofanyika na hasa kuondolewa kwa wawakilishi wa wagombea 12 wa kiti cha rais kutoka vituo vya kupiga kura.
Mpigaji Kura
Sijambo la haki kwa vile ukiitisha uchaguzi inabidi kuheshimu utaratibu kamili, kwani wasimamizi wa wagombea wa upinzani wanafuatilia uchaguzi kwa niaba yao. Sasa vipi tutasema ni uchaguzi wa haki ikiwa wagombea hawana wafuatiliaji wao, walisema baadhi ya wapiga kura.
Akipiga kura katika mji alikozaliwa Mitsoudje, Rais Azali aliyekataa kujiuzulu lakini hakusema anachukuwa likizo kwa ajili ya uchaguzi, aliwambia waandishi habari baada ya kupiga kura kwamba alipata habari za ghasia zilizotokea, lakini hilo ni jambo la kawaida.
Kauli ya Rais
Azali assoumani Rais wa Comoros amesema: " Nimeambiwa kulikuwepo na matatizo hapa na pale hilo ni jambo la kawaida, na kwamba wote polisi na tume ya uchaguzi wamechukuwa hatua zinazohitajika. Ikiwa kuna masanduku yaliyojazwa kura yanaweza kuondolewa na mengine yakapelekwa."
Kuna karibu wapiga kura laki 3 waliojiandikisha lakini tatizo jingine lililojitokeza ni kwamba kulikuwepo na ripoti za majina ya watu wengi waloidhinishwa na mahakama kuwakilishwa na mtu mwengine kuwapigia kura, ikiwa hawatoweza kufika katika kituo cha kupiga kura.
Wasemavyo wapinzani
Upinzani unasema idadi imekuwa kubwa kupita kiasi na inatia wasi wasi kuwa ni njama kubwa ya wizi unaofanywa na serikali.
Mahamoudou Ahmada moja wapo wa wagombea wa upinzani anasema serikali imefanya mapinduzi katika uchaguzi.
Mahamoudou Ahamada, mgombea kiti cha rais chama cha Juwa anasema , "Mimi ninachukulia Jumuia ya kimataifa ndiyo mashahidi wakuu. Nimewaarifu tangu jana kwamba nimewasiliana na tume ya uchaguzi tangu jana na kuwaelezakwamba wawakilishi wangu hawajaruhusiwa kuingia ndani ya vituo vya kupiga kura kuniwakilisha."
Hadi Jumatatu jioni
Kufika Jioni wagombea wote 12 walikutana na kutoa taarifa ya kuwataka wafuasi wake kuzuia masanduku ya kura kuwasilishwa katika jengo la bunge ambako tume ya uchaguzi imeweka makao yake makuu ya kuhesabia kura. Wafuasi wa upinzani hawakuitikia wito wa jana kwa hofu ya kuzuka ghasia na wagombea walipojaribu kwenda bungeni walizuiliwa na kikosi cha kupambana na ghasia na hawakuweza kufanya chochote.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC