Nigeria: Polisi watangaza marufuku ya kutoka nje katika jimbo la Kano

Raia wa Nigeria wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

Jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Kano, Jumatano lilitangaza marufuku ya kutoka nje ya saa 24, baada ya mahakama kubatilisha uchaguzi wa mgombeaji wa upinzani kama gavana, na kumtangaza mfuasi wa chama cha Rais Bola Tinubu kuwa mshindi halali.

Polisi wa Kano, jimbo ambalo lina idadi kubwa zaidi ya wapiga kura waliojiandikisha, walisema katika taarifa kwamba wanaokiuka amri ya kutotoka nje "watakamatwa na kukabiliwa vikali kisheria."

Kabla ya uamuzi wa mahakama ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilichukua udhibiti wa barabara kuu, katika mji mkuu wa Kano.

Magavana wana ushawishi mkubwa nchini Nigeria, wakisimamia bajeti kubwa kuliko baadhi ya nchi ndogo za Afrika, na umaarufu wao mara nyingi huchangia pakubwa kuhusiana ni nani atakuwa rais.

Uamuzi wa Jumatano wa jopo la majaji watano ulizusha hofu ya kutokea machafuko katika jimbo hilo lenye Waislamu wengi. Kura ya ugavana mwezi Machi ilishuhudia Abba Yusuf wa New Nigerian Peoples Party, chama cha kikanda, akimshinda mgombea wa chama tawala cha All Progressives Congress, Nasiru Gawuna, ambaye alidai kwamba zoezi hilo liligubikwa na udanganyifu.

Yusuf anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama katika Mahakama ya Juu. Sio kawaida kwa matokeo ya uchaguzi wa ugavana kupinduliwa nchini Nigeria, ambayo ina majimbo 36 ambayo yanasimamiwa na serikali za majimbo.