Ndege iliyombeba rais wa Iran Ebrahim Raisi yaanguka

Rais wa Iran Ebrahim Raisi.

Helikopta iliyokuwa imembeba rais wa Iran Ebrahim Raisi na waziri wake wa mambo ya nje ilianguka siku ya Jumapili ilipokuwa ikivuka eneo la milima katika ukungu mkubwa, wakati ikirejea kutoka kwenye mpaka na Azerbaijan, afisa mmoja wa Iran aliliambia shirika la habari la Reuters.

Afisa huyo alisema maisha ya Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian "yako hatarini kufuatia ajali ya helikopta".

"Bado tuna matumaini lakini taarifa zinazotoka kwenye eneo la ajali zinatusumbua sana," afisa huyo alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

Hali mbaya ya hewa ilikuwa ikitatiza juhudi za uokoaji, shirika la habari la serikali IRNA liliripoti.

Televisheni ya Taifa ilisimamisha programu zake zote za kawaida ili kuonyesha maombi yakifanywa kwa ajili ya Raisi kote nchini na, katika kona ya skrini, matangazo ya moja kwa moja ya timu za uokoaji katika eneo la milimani lenye ukungu mzito.

Raisi, mwenye umri wa miaka 63 alichaguliwa kuwa rais katika jaribio la pili mwaka 2021, na tangu aingie madarakani ameamuru kuimarishwa kwa sheria za maadili, kusimamia ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya maandamano ya kupinga serikali na kusukuma vikali mazungumzo ya nyuklia na mataifa yenye nguvu duniani.

Katika mfumo wa kisiasa wa Iran, uliogawanyika kati ya taasisi ya viongozi wa kidini na serikali, ni kiongozi mkuu badala ya rais ndiye mwenye sauti ya mwisho kuhusu sera zote kuu.

Lakini wengi wanamuona Raisi kama mshindani mkubwa wa kumrithi mshauri wake mwenye umri wa miaka 85, Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, ambaye ameidhinisha vikali sera kuu za Raisi.

Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmed Vahidi aliiambia TV ya serikali kwamba moja ya helikopta katika ya tatu zilizokuwa zikipaa katika eneo hilo ilianguka kwa kishindo, na kwamba mamlaka inasubiri maelezo zaidi.

Raisi alikuwa kwenye mpaka wa Azerbaijan kuzindua Bwawa la Qiz-Qalaisi, mradi wa pamoja.