Maafisa wa NATO wamesema Jumamosi kwamba uchunguzi unafanyika kutokana na madai kwamba kombora kutoka ndege za ushirika limepiga mlolongo wa magari ya wapiganaji wa Libya karibu na mji wa mafuta wa mashariki wa Brega na kusababisha vifo vya watu 10.
Mashahidi wanasema mtu mmoja katika kundi la wapiganaji alifyatuwa hewani mizinga ya kushambulia ndege muda mfupi kabla ya shambulio hilo usiku wa Ijumaa.
Lakini haijulikani wazi ikiwa mizinga ilifyatuliwa na waasi waliokuwa wanasherehekea ushindi au wanajeshi wa Moammar Gadhafi waliopenya na kujiunga na kundi la wapiganaji.
Mashahidi wanasema waliona angalau magari manne yaliyokuwa yanawaka moto baada ya shambulio la Ijumaa.
Mlolongo wa magari hayo yalikuwa yanaelekea Brega, moja wapo ya miji kadhaa ya mafuta kwenye pwani ya Mediterranean ambayo imekuwa ikidhibitiwa mara na waasi mara na wanajeshi wa serikali tangu mapigano kuanza kati kati ya mwezi wa Februari.