Museveni aapishwa, Besigye arejea nchini

Kiongozi wa upinzani Kiiza Besigye, akihutubia wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mapema mwaka huu.

Marais wa nchi jirani wahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Museveni kushika awamu ya nne ya uongozi

Rais Yoweri Museveni ameapishwa kushika awamu ya nne ya uongozi wake nchini Uganda Alhamisi huku mpinzani wake mkuu Kizza Besigye akirejea nyumbani na kupokelewa kwa shangwe kubwa baada ya kupata matibabu nchini Kenya.

Museveni, mwenye umri wa miaka 66, na ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 alikula kiapo mbele ya maelfu ya wananchi na viongozi kadha wa nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na nchi jirani za Tanzania, Kenya na Zimbabwe.

Wakati huo huo, maelfu ya watu walijitokeza kumkaribisha nyumbani kiongozi wa upinzani Besigye ambaye alishindwa na Museveni katika uchaguzi wa Februari 18 ambao wapinzani walidai kuwa na wizi wa kura.

Besigye ambaye ameshindwa na Museveni mara tatu katika uchaguzi wa urais Uganda aliwasili kutoka Nairobi ambako alikaa kwa muda wa siku kadha kupata matibabu baada kufuatia majeraha aliyopata katika maandamano ya upinzani mjini Kampala mwezi uliopita.