Kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye amesema amezuiwa kupanda ndege kutoka Kenya kurudi Uganda siku moja kabla ya kuapishwa kwa rais Yoweri Museveni kuongoza muhula wake wa nne.
Besigye alisema leo kuwa afisa mmoja wa shirika la ndege la Kenya alimwambia serikali ya Uganda haitairuhusu ndege hiyo kutua ikiwa itamchukua Besigye atakuwa ndani ya ndege hiyo.
Lakini afisa mmoja wa Uganda alikanusha tuhuma hizo akisema serikali haihusiki kabisa na suala hilo.
Besigye alikuwa Nairobi kwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata katika mapambano na Polisi wakati akishiriki kwenye maandamano ya kupinga kupanda kwa bei za chakula na mafuta ya petroli.
Watu wapatao 8 wameuwawa na zaidi ya 250 kujeruhiwa wakati wa wiki kadhaa za maandamano ya upinzani.
Bw. Museveni ametetea hatua za majeshi ya usalama na kuapa kuzima maandamano. Amelaumu kupanda kwa gharama za maisha kunatokana na ukame na ongezeko la bei za mafuta.