Mwili wa mtanzania mhandisi wa Google wapatikana kwenye mto Miami

Abraham Mgowano. Picha imetolewa kutoka katika matangazo ya Televisheni ya WSVN

Mwili wa raia wa Tanzania umepatikana ukielea katika Mto Miami Marekani Jumanne asubuhi na idara husika zikithibitisha kuwa mwili huo ni wa mtu aliyeanguka kutoka katika mashua mwishoni mwa juma.

Mwili wake ulipatikana ukieleya katika mto Miami karibu na daraja lililopo kwenye mtaa wa 2nd Street, Northwest.

Picha zilizopigwa kutoka kwenye helikopta zilionyesha boti ya Uokoaji wa Moto ya Miami ikielekea kwenye tukio na kuuondoa mwili huo kutoka majini.

Maafisa wa Polisi wa Miami walithibitisha mwili huo ni wa Abraham Mgowano, ambaye aliripotiwa kupotea siku ya Jumamosi mchana.

Mgowano ambaye alikuwa na umri wa miaka 35, alifanya kazi katika kampuni ya Google kama mhandisi wa program za komputa.

Kwa mujibu wa Idara ya kuhifadhi viumbe vya majini na Wanyamapori ya Florida, FWC Mgowano ni mkazi wa Berkley, California, ni alikuwa mmoja wa abiria 12 kwenye mashua ya kifahari yenye urefu wa futi 44 kabla ya kuanguka mtoni mwendo wa saa 2:30 usiku. Maafisa wa FWC wanasema uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na ajali hiyo.

​Vyanzo vya habari hii ni Kituo cha Televisheni cha CBS News na WSVN