Afisa wa zamani wa polisi Fulgence Kayishema amekuwa mafichoni tangu mwaka 2001, wakati Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji kwa Rwanda (ICTR) ilipomfungulia mashtaka ya mauaji ya kimbari kutokana na jukumu lake kwa uharibifu uliofanyika katika Kanisa Katoliki la Nyange lililoko katika Jimbo la Kibuye.
"Kukamatwa kwake hatimaye kunahakikisha kuwa haki itatendeka kuhusiana na shutuma kwa uhalifu wake," mwendesha mashtaka Serge Brammertz katika mahakama ya kimataifa ya utaratibu wa mabaki kwa mahakama za uhalifu (IRMCT), ambao umechukua nafasi ya ICTR tangu ilipofungwa mwaka 2008.
Kayishema anatarajiwa kuhamishiwa Rwanda kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka wakati Umoja wa Mataifa umesema mwaka 2012 kesi yake ilipelekwa kwa mamlaka ya Rwanda.
Akitoa maoni yake mara baada ya kukamatwa kwa Kayishema, msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo aliandika katika mtandao wa Twitter: "Hatimaye."
Inakadiriwa kuwa watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, yaliyoratibiwa na utawala wa kihutu uliokuwa na msimamo mkali, na kutekelezwa na maafisa wa kieneo na raia wa kawaida katika jamii yenye matabaka ya juu.
Kayishema alikuwa katika orodha ya watu wanaotafutwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani chini ya Mpango wa Tuzo kwa Haki, na tuzo ya dola millioni tano kutolewa kwa atakayesaidia kukamatwa kwake.
Brammertz alisema uchunguzi uliopelekea kukamatwa kwake ulisambaa katika nchi kadhaa barani Afrika na kwingineko, na iliwezekana kupitia msaada na ushirikiano wa mamlaka za Afrika Kusini.
Mwezi Mei mwaka 2020, mhusika mwingine mkuu aliyepanga mauaji ya kimbari, Felicien Kabuga, alikamatwa nchini Ufaransa baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 26.
Kukamatwa kwa Kayishema sasa kunamaanisha kuna watuhumiwa watatu waliobaki mafichoni wanaoshitakiwa na mahakama ya kimataifa ambao bado hawajulikani walipo, ingawa msemaji wa serikali ya Rwanda amesema wanafikiria kuwa idadi kubwa ya washukiwa bado wako mafichoni.