"Malori hayo yanahitaji kusafiri haraka iwezekanavyo kwa njia kuu ya moja kwa moja na ambayo ni salama kutoka Misri hadi Gaza," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliuambia mkutano wa kilele wa amani mjini Cairo Jumamosi.
Aliishukuru Misri kwa mchango wake katika kuwezesha msafara huo.
"Lakini watu wa Gaza wanahitaji misaada zaidi – utoaji mfululizo wa misaada kwa Gaza kwa kiwango kinachohitajika," alisema Guterres.
"Tunafanya kazi bila kukoma na wahusika wote ambao ni muhimu kufanikisha hilo," aliongeza.
Darzeni za malori yalikuwa yamejipanga karibu na Rafah kwa siku kadhaa yakisubiri mpaka kufunguliwa ili kupelekamsaada kwa wakazi zaidi ya milioni 2 wa Gaza.
Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alisema katika taarifa yake kwamba "vifaa vya kuokoa maisha" katika msafara huo vinatolewa na Shirika la Hilali Nyekundu ya Misri na Umoja wa Mataifa. Alisema wameidhinishwa kuvuka Gaza na kupokelewa na Hilali Nyekundu ya Palestina, kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.
Msafara wa Jumamosi ni mara ya kwanza kwa msaada huo kuruhusiwa kuingia Gaza tangu Hamas ilipofanya shambulizi la kushtukiza dhidi ya Israeli Oktoba 7 na kuua watu wapatao 1,400, na kusababisha kampeni ya Israeli ya kulipua mabomu na kuziba kabisa Gaza. Zaidi ya Wapalestina 4,000 wameuawa. Gaza sasa inajiandaa kwa uvamizi wa ardhini wa Israeli.
Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza mpango huo wa msaada mdogo kwa Gaza wakati wa ziara yake mjini Tel Aviv siku ya Jumatano, lakini utekelezaji ulicheleweshwa huku Umoja wa Mataifa ukifanya kazi na Misri, Israeli na Marekani kutathmini hali ilivyo na kupunguza vikwazo vilivyowekwa.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limesema malori yake matatu yalikuwa sehemu ya msafara huo. Yalibeba tani 60 za chakula cha dharura, ikiwa ni pamoja na chakula cha mkebe, unga wa ngano na pasta. WFP ina tani nyingine 930 za chakula cha dharura kwenye au karibu na kivuko cha Rafah, tayari kupelekwa twa Gaza wakati wowote ufikiaji utakaporuhusiwa tena.
"Chakula hiki kinahitajika sana kwani hali ndani ya Gaza ni mbaya sana. Malori haya ishirini ni hatua muhimu ya kwanza, lakini msafara huu unapaswa kuwa wa kwanza kati ya mingi mingine,” Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain alisema katika taarifa.
Shirika la Afya Ulimwenguni limesema lilikuwa na malori manne yaliyokuwa yakielekea Gaza yakiwa yamebeba vifaa vya kutibu magonjwa sugu, dawa za kutibu magonjwa sugu, dawa muhimu na vifaa vya afya. Inasema ina vifaa zaidi nchini Misri vinavyoelekea Gaza.
"Vifaa vinavyoelekea Gaza hivi sasa havitoshi kushughulikia mahitaji ya kiafya yanayoongezeka huku uhasama ukiendelea kuongezeka," WHO ilisema katika taarifa. "Operesheni ya misaada iliyoimarishwa na kulindwa inahitajika sana."
Ubalozi wa Marekani nchini Israeli ulionya kwamba raia yeyote wa kigeni anayejaribu kuondoka Gaza wakati kivuko cha mpaka kikiwa wazi "watarajie mazingira yanayoweza kuwa ya fujo katika pande zote mbili za kivuko hicho."