Moto wauwa watu wasiopungua 27 Istanbul

Wazima moto wakizuia moto kusambaa katika eneo lililowaka moto kwenye jengo la makazi ya watu huko Istanbul Aprili 2, 2024.

Moto katika klabu  ya starehe ya usiku mjini Istanbul, Uturuki wakati ikifanyiwa ukarabati Jumanne umeuwa watu wasiopungua 27, maafisa na taarifa mbalimbali zimesema.

Watu kadhaa, wakiwemo mameneja wa klabu hiyo, walishikiliwa na polisi kuhojiwa.

Mtu mmoja anatibiwa hospitali, ofisi ya gavana wa Istanbul ilisema katika taarifa.

Klabu hiyo ya Masquerade, ambayo ilifungwa kwa ajili ya ukarabati, ilikuwa katika eneo la chini ya ardhi na juu ya ardhi ya jengo lenye ghorofa 16 ya jumba la makazi ya watu katika wilaya ya Besiktas upande wa Ulaya wa mji uliotenganishwa na eneo la Bosphorus. Moto huo ulizimwa.

Gavana Davut Gul aliwaambia waandishi wa habari katika eneo la tukio kuwa chanzo cha moto huo kinachunguzwa na waathirika walisadikiwa kuhusika katika shughuli za ukarabati.

Mamlaka imewakamata watu watano kwa ajili ya kuwahoji, wakiwemo mameneja wa klabu hiyo na mtu mmoja aliyekuwa ana jukumu la kufanya ukarabati huo, Waziri wa Sheria Yilmaz Tunc alisema.

Meya Ekrem Imamoglu alisema mamlaka zilikuwa zinakagua jumba kutathmini usalama wake.

Wazima moto kadhaa na timu ya madaktari wamepelekwa katika eneo la tukio hilo, alisema.