Beki Nou-haila Benzina alikua mchezaji wa kwanza kuvaa Hijab katika mchezo wa Kombe la Dunia katika kiwango cha juu, na mwenzake Ibtissam Jraidi alifunga bao la kwanza la timu ya Atlas Lionesses katika Kombe la Dunia.
Wamorocco walifunga katika dakika ya 6 na kupambana hadi mwisho wa mechi bila kufungwa bao lolote na wapinzani wao.
Baada ya kushindwa na Ujerumani kwa mabao 6 kwa 0, ushindi huo wa Jumapili unaifanya Morocco iliyo katika nafasi 72, kupata fursa ya kuendelea kwa hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
Morocco linakuwa taifa la kwanza la Kiarabu kuwahi kushinda katika Kombe la Dunia la Wanawake na kufikia Jumapili, bado ilikuwa na nafasi ya kuingia katika kinayan'anyiro cha 16 bora.
Uwezekano wa Korea Kusini kuondolewa kwenye michuano hiyo ulikuwa mkubwa baada ya kupoteza kwa mara ya pili.
Nini kitafuata?
Morocco itamenyana na Colombia siku ya mwisho ya hatua ya makundi Alhamisi mjini Perth katika mechi ambayo huenda ikaamua ni timu gani kati ya hizo mbili itafuzu kwa hatua ya 16.
Korea Kusini itacheza na Ujerumani mjini Brisbane. Mechi hizo mbili zitaanza kwa wakati mmoja.