Mkuu wa wafanyakazi wa rais Madagascar akamatwa London kwa tuhuma za kutaka hongo

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina alipotangazwa kuwa rais Machi 21, 2009. Picha na REUTERS/Siphiwe Sibeko.

Mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Madagascar amekamatwa mjini London baada ya kushukiwa kutaka hongo kutoka kwa wachimbaji wa madini ya thamani ya Gemfields, Shirika la Kitaifa la Uhalifu la Uingereza (NCA) lilisema Jumatatu.

Romy Andrianarisoa, ambaye anafanya kazi kwa Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, alikamatwa akiwa pamoja na raia wa Ufaransa ambaye ni mshiriki katika mkutano uliokuwa ukifanyika mjini London ambapo shirika hilo la uhalifu la NCA limesema wanaaminika walikuwa wakijaribu kutaka hongo ili kutoa leseni za kufanya kazi katika taifa hilo lililopo katika kisiwa cha Afrika.

Si msemaji kutoka ofisi ya rais Rajoelina wala wawakilishi wa washukiwa hawakuweza kupatikana mara moja.

NCA ilisema kuwa wawili hao walikuwa wakiomba rushwa ya takriban dola 286,000 kwa ajili ya malipo ya awali pamoja na hisa ya asilimia tano.

"Ninaishukuru Gemfields kwa kutuletea jambo hili na kwa ushirikiano wao unaoendelea wakati wa uchunguzi," mkuu wa kitengo cha kimataifa cha rushwa cha NCA, Andy Kelly, alisema katika taarifa.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la Reuters