Mkutano wa G20 wafunguliwa Argentina

Viongozi wa mataifa 20 yaliyo endelea katika viwanda yanayo fahamika kama G20 wanaanza mkutano wao wa siku mbili Ijumaa mjini Buenos Aries, Argentina.

Wakati huo huo mivutano inaendelea inayo sababishwa na Rashia katika mvutano wake na Ukraine na msimamo thabiti wa Rais Trump juu ya uhusiano wa bishara na China na kukana kwake mabadiliko ya hali ya hewa.

Viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia masuala ya uchumi, mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji, na masuala mengine muhimu katika mkutano huo.

Pembani ya mkutano mkuu kutakuwepo na mazungumzo ya nchi na nchi pamoja na mikutano ya kikanda ambapo asubuhi ya leo Rais Trump pamoja na rais mwenzake wa Mexico Enrique Pena Nieto na waziri mkuu wa Canada Pierre Trudeau wametia saini mikataba mpya ya biashara kati ya nchi zao tatu unaofahamika sasa kama USMCA, iliyokuwa ikifahamika awali kama NAFTA.

Viongozi wa umoja wa ulaya wamekutana kujadili pia namna ya kuzuia sera za Rais Trump za kujitenga kibiashara na kususia mikataba ya kimataifa.

Kwa upande mwengine Rais Trump amefutilia mbali mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Rashia kabla ya kuwasili Argentina lakini ataendelea kukutana na Rais Xi Jingping wa China hapo kesho kuzungumzia mvutano wao wa kibiashara wakieleza matumaini ya kufikia makubaliano .

Mwanamfalme mrithi wa Saudia Arabia Mohammed Bin Salman anahudhuria mkutano huo na itakua ni mara ya kwanza kwa viongozi wa dunia kukutana naye baada ya mauwaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi, aliyeuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul.

Nje ya ukumbi wa mkutano wanaharakati wamepanga kufanya maandamano mchana wa leo saa za Argentina kupinga sera za biashara za kimataifa na hasa matatizo ya kiuchumi ya Argentiuna nan chi za Amerika ya kusini.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC