Wakizungumza na Sauti ya Amerika, katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, baadhi ya wadau wameitaka jamii, kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ambayo vijana wengi hutumia muda mwingi zaidi katika kupata na kusambaza habari.
Mwandishi wa habari wa Capital FM Nairobi Moses Muoki, amesema elimu na ubunifu unahitajika ili kuwalenga vijana kupitia mitandao ya kijamii ambayo imechangia katika kuiangalia ngono kuwa jambo la kawaida.
Francis Jonson, mfanyakazi wa kituo cha Wazee huko Tanga, amesema jamii ielekeze nguvu katika mitandao kwa lengo la kuwaelimisha vijana ambao hutumia “mitandao kwa kipindi kirefu kuliko wanavyoongea na marafiki zao” alisema.
Baadi ya wanaharakati na wadau wamesema kutokana na utandawazi uliopo, vijana wengi wamekuwa wakiitumia vibaya mitandao ya kijamii na kuiga maadili na tabia ambazo haziendani na maadili ya jamii zao.
Tedy Mmbaga, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, anasema jamii inapaswa kuelimishwa jinsi ya kuitumia mitandao katika misingi wa kuwanuifaisha. Vijana “wanaiga kwenye mitandao, wanawaangalia watu wa Magharibi wanavyoishi, na ile inawashawishi vijana wengi” Alisema Tedy
“Mitandao ya kijamii inachochea kwa kiwango kikubwa vijana kufanya mambo mabaya , wanaiga kwenye mitandao, wanawaiga watu wa nchi za Magharibi wanavyoishi na ile inawashawishi vijana wengi” alisema Maria Msaada, Mkurugenzi wa Taasisi ya watoto yatima ya Voice of Ophans iliyoko Tanzania
Wakizungumzia sheria za mitandao, walizitaka mamlaka kufuatilia sheria za mitandao ili kudhibiti kuporomoka kwa maadali ikiwemo usambazaji wa picha za ngono mitandaoni.