Miili 17 yapatikana baada ya maporomoko ya matope Uganda

Ramani ya Uganda

Idadi isiyo julikana ya watu wamepoteza maisha kufuatia maporomoko ya matope katika wilaya ya Bududa mashariki mwa Uganda karibu na mlima Elgon, katika kile maafisa wanataja kuwa ni maporomoko makubwa na hatari kuwahi kushuhudiwa.

Mbunge wa zamani wa Manjiya

“Mvua ilikuwa si nyingi. Ilikuwa ya kawaida tu. Lakini maji yalitoka mlimani kwa kasi sana na kuharibu kila kitu kilicho kuwa kwenye mkono yaliyo fuata. Matope, mchanga na kila kitu kilichong’olewa na maji kimewafunika watu. Hadi sasa tumepata maiti 17 lakini hatujajua idadi kamili ya walio kufa” amesema David Wakikona, mbunge wa zamani na mkazi wa Kaunti ya Manjiya.

Wakikona ameiambia Sauti ya Amerika kwenye mahojiano ya simu kwamba maporomoko ya matope yalianza baada ya maji yenye msukumo wa kasi sana kufoka kutoka kwenye chemuchemu juu ya mlima.

Wakazi wa Bududa

Kwa mujibu wa wakazi wa wilaya ya Bududa, kata ndogo ya Bukalasi, yenye milima mingi, maporomoko ya matope yalianza kushuhudiwa saa nane alasiri, wakati maji, matope, na miti ikiporomoka kutoka juu ya mlima, kufunika makao ya watu hadi sehemu tambarare madukani.

Hadi tukiandaa taarifa hii, maafisa wa uokoaji walikuwa hawajafika eneo la tukio, wakazi wa eneo hilo wenye ujasiri wakijitwika jukumu la kuwaokoa wenzao.

“Nyumba zimefunikwa na udongo. Kituo cha kibishara nacho kimefunikwa kiasi kwamba huwezi kujua kama kilikuwepo. Kwa sasa tunaogopa kuwaokoa wenzetu kwa sababu huwezi kujua, maporomoko makubwa Zaidi yanaweza kutokea tena,” ameongezewa Wakikona.

Shirika la Msalaba Mwekundu

Taarifa fupi ya msemaji wa shirika la msalaba mwekundu nchini Uganda, Irene Nakasita, imethibitisha tukio hilo na kusema kwamba huenda idadi ya vifo ikawa kubwa sana, ikiongezea kwamba kuna hali ya wasiwasi mkubwa katika wilaya nzima ya Bududa, wakati huu wa mvua.

Juhudi zetu za kumpata waziri wa majanga wa Uganda Musa Echweru hazikufaulu.

“matope yamefunika sehemu kubwa sana. Kutoka Bukalasi hadi Nalwzanza. Ni mbali sana. Ni sehemu kubwa sana imefunikwa. Tuna hofu kwamba mvua ikiendelea kunyesha au ikiongezeke, basi maporomoko Zaidi yanaweza kushuhudiwa,” amesema Wakikona

Zaidi ya watu 100 walikufa baada ya kutokea maporopoko ya ardhi katika wilaya hiyo ya Bududa mwaka 2010.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, Sauti ya Amerika, Washington DC